Watu kutoka mji wa Wete Zanzibar wakinunua chakula sokoni. Bei za chakula zilipanda karibuni hadi kufikia asilimia 100 kutokana na kubadilikabadilika kwa bei za fedha za kigeni.
Kubadilikabadilika kukubwa kwa bei za chakula ambako Tanzania imeshuhudia katika miezi ya karibuni ni ishara kwamba uchumi wa nchi haukutengamaa kimuundo, wanauchumi wasema.
Baada ya bei za chakula kushuka kwa muda mfupi kutokana na kukaribia kwa msimu wa mavuno wa mwezi Oktoba, zilipaa tena mwezi wa Novemba baada ya nchi kukumbwa na uhaba wa mafuta.
Kwa mujibu wa data zilizotolewa tarehe 23 Novemba na Wizara ya Viwanda na Biashara, baadhi ya bei za mazao zilipanda hadi kufikia asilimia 100 katika wiki za mwanzo za mwezi huu.
Kwa mfano, mjini Dar es Salaam, bei kwa kila kilo moja ya maharage ilipanda kutoka shilingi 600 (senti 37 za dola) hadi shilingi 1,200 (senti 75 za dola), bei ya mahindi ilipanda kutoka shilingi 600 (senti 37 za dola) hadi shilingi 700 (senti 44 za dola), mchele kutoka shilingi 1,600 (dola 1) hadi shilingi 2,200 (dola 1.37) na unga wa ngano kutoka shilingi 600 (senti 37 za dola ) hadi shilingi 900 (senti 56 za dola).
Ili kujilinda dhidi ya kuanguka kwa bei ya shilingi, Watanzania wengi wanategemea dola ya Marekani na pesa nyengine za kigeni kwa ajilli ya kununua na kuuza bidhaa, utaratibu ambao unazidisha kuiyumbisha pesa ya nchi na kusababisha kupaa kwa bei za chakula, kwa mujibu wa Mushengezi Nyambele, mchumi na katibu wa zamani wa bodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania.
"Hata watu wa kawaida wamepoteza imani na fedha yetu," aliiambia Sabahi. "Wote wanachagua dola, jambo ambalo husababisha uhaba wa dola nchini, na kwa hivyo kuchochea kuongezeka kwa bei." Alisema kuwa mafuta yanapanda kwa sababu mzunguko mdogo wa dola nchini Tanzania, badala yake kuathiri bei za bidhaa na huduma.