
Zitto
Kabwe
TAMASHA
LA MATUMAINI-DAR-ES-SALAAM
Leo
(JANA)nilikuwa niwe nanyi kwa ajili ya siku hii muhimu sana kwa nchi yetu, siku ya
matumaini kama inavyoandaliwa na Kampuni ya Global Publishers. Napenda kutoa
shukrani zangu za dhati kabisa kwa ndugu yangu Erick Shigongo kwa kuandaa
tamasha hili kila mwaka. Nasikitika kuwa sitaweza kufanya pambano la ngumi na
ndugu Ray na pia kuchezea timu yangu ya Wabunge wa Simba dhidi ya watani zetu
Yanga. Hata hivyo naamini kuwa tamasha litakuwa na mafanikio makubwa na nipo
nanyi japo sipo Dar es Salaam.
Ilikuwa
niwepo Dar es Salaam leo, lakini nimeshindwa kuondoka Marekani kwa sababu Spika
wa Bunge Mama Anna Makinda ameniagiza kwenye safari nyingine ndefu kwenda
visiwa vya Cayman na baadaye Namibia kwa shughuli za Umoja wa Wabunge wa
Jumuiya ya Madola. Sikuweza kukwepa jukumu hili la kitaifa maana limekuja
ghafla na mimi nipo huku jirani na maeneo hayo. Naomba radhi sana kwamba sipo
nanyi leo.
Nawaomba
muiombee amani nchi yetu na msimamie haki kwa wananchi wote bila kubagua dini
zao, rangi zao, hali yao kimaisha na ufuasi wa vyama vya siasa. Mwaka huu
tumeshuhudia matukio ambayo yanatikisa msingi wa Taifa letu – Umoja. Hivi sasa
msingi wetu una nyufa ambazo kwa kweli hatujajua bado nini kinacholeteleza
mambo haya kama kulipua makanisa, kulipua mikutano ya vyama vya siasa na kuua
viongozi wa dini.
Matukio
haya yanatuelekeza kuwa makini sana na kauli zetu kwani baadala ya kuunganisha
wananchi tunawezajikuta tunawagawa zaidi Watanzania na hivyo kuwa na mzunguko
wa machafuko (vicious circle of violence). Ni wajibu wa viongozi wa kisiasa na
wananchi kuepuka kabisa kuanza kurushiana maneno na lawama kuhusu matukio haya,
kwani inawezekana lawama na maneno yetu yakawa yanampa nguvu adui wetu ambayo
hatujamjua bado.
Napenda
niwakumbushe kwamba ni rahisi sana kusambaza chuki na ni vigumu sana kuondoa
chuki miongoni mwa wananchi. Viongozi hatari kama Hitler walitumia sana mbinu
ya kueneza chuki dhidi ya jamii ya Jews na matokeo yake yalikuwa ni vita vikuu
vya pili vya dunia na zaidi ya watu milioni 6 wasio na hatia kupoteza maisha.
Sisi sote tuna jukumu moja la kuhakikisha tunajenga Taifa lenye kujali HAKI na
lenye mshikamano mkubwa miongoni mwa raia. Kwa nia hii tu ndio tutaweza kuwa na
Taifa imara lenye heshima mbele ya mataifa mengine duniani.
Ni kwa njia hiyo tu
ndio tutaweza kutokomeza umasikini uliokithiri mijini na vijijini hapa nchini
kwa kuongeza uzalishaji na kupanua ajira. Ikumbukwe bila HAKI hakuna AMANI na
bila UWAJIBIKAJI hakuna UTULIVU.
Tukiegemea
siasa za CHUKI. Tukashindwa kuwa na mahusiano ya kawaida miongoni mwa viongozi
kuhusu masuala ya msingi ya nchi. Tukashindwa kujadiliana kwa hoja kuhusu sera
zetu. Tutapata viongozi aina ya Hitler nchini mwetu. Wote tukatae. Sisi ni
Watanzania. Muwe na Tamasha jema la Matumaini.
Zitto
Kabwe
7.7.2013,
Aspen Colorado, USA.
No comments:
Post a Comment