April 15, 2014
THE UNITED REPUBLIC OF
TANZANIA
DIRECTORATE OF
PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Telephone:
255-22-2114512, 2116898
E-mail:
ikulumawasiliano@yahoo.com
press@ikulu.go.tz
Fax: 255-22-2113425
PRESIDENT’S OFFICE,
THE STATE HOUSE,
P.O. BOX 9120,
DAR ES SALAAM.
Tanzania.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA
HABARI
TAMKO LA KATIBU MKUU
KIONGOZI KWA VYOMBO VYA HABARI
KUHUSU HATI YA MUUNGANO
WA TANGANYIKA NA ZANZIBAR
IKULU, DAR ES SALAAM,
TAREHE 14 APRILI, 2014
__________________________________________________
Siku 12 zijazo
tutasherehekea miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, na kuzaliwa kwa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania. Wamezaliwa watu ndani ya Muungano huu na wengine wana
wajukuu.
Inasikitisha sana kuwa
leo, miaka 50 baadaye ipo dhana potofu inayojengwa kuwa Muungano huu si halali
kwa vile hakuna Hati ya Muungano (Articles of the Union).
Waasisi wa Taifa letu
ambao tarehe 22 Aprili, 1964 kule Zanzibar walitia saini Hati hiyo, mbele ya
mashuhuda, nao wameonekana kama walichokifanya kilikuwa kiini macho, na kwa
hiyo kwamba waliongoza Taifa jipya la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa msingi
wa kiini macho hicho kwa miaka yote hadi Mwenyezi Mungu alipowaita.
Mambo yote mawili
yametusononesha sana sisi Serikalini, na bila shaka yamewasononesha wananchi
wanaoipenda nchi yao, wanaowapenda Waasisi wa Taifa letu na kuuenzi Muungano
wao.
Madai ya kuonyeshwa
Hati ya Muungano yalianza siku nyingi lakini hatukuweza kuamini hali itafikiwa
ilipofikia, ambapo wapo watu wanathubutu kudai na kuapa kuwa Hati hiyo haipo.
Ukweli ni kuwa hati
hiyo ipo, ilikuwepo siku zote. Hata hivyo, lazima tukubaliane kuwa zipo Hati
fulani ambazo ni kiini cha uwepo wetu kama Taifa huru, Jamhuri huru na Muungano
huru, ambazo tunazihifadhi kama mboni ya jicho. Hati hizo ni pamoja na Hati ya Uhuru
wa Tanganyika ya mwaka 1961, Hati ya Tanganyika kuwa Jamhuri mwaka 1962, na
Hati ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ya mwaka 1964. Hati za aina hii
zinahifadhiwa maeneo maalum ambayo ni salama ili zisipotee wala kuharibika. Kwa
kawaida hatuzitoi, tunazifungua ili kuzihifadhi kwa namna yoyote ile.
Lakini sasa maneno
yanakua mengi, tuhuma zimekuwa nyingi, dhihaka zimekuwa nyingi, kiasi cha
wananchi kuanza kutiwa mashaka iwapo kweli Hati ya Muungano ipo au la.
Hivyo, kwa maagizo na
ridhaa ya Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, ninaleta mbele yenu Hati ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
iliyotiwa saini Zanzibar na waasisi wetu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na
Mzee Abeid Aman Karume, ili muione na kuwahakikishia Watanzania kuwa
yanayosemwa kuwa hakuna Hati hiyo si kweli. Hati hiyo ipo tangu wakati huo,
imetunzwa vizuri na waliotutangulia, tumeirithi, na tutaendelea kuihifadhi.
Na, tukiombwa kufanya
hivyo na Mwenyekiti wa Bunge Maalum nina uhakika Rais ataridhia ipelekwe huko
ili kuondoa mjadala wa kama Hati ipo au la.
Isitoshe, tufanye
utaratibu wa kuweka nakala kwenye Makumbusho ya Taifa ili kila atakayetaka
kuiona katika miaka mingine 50 ijayo na kuzidi aione.
Mwisho, narejea kusema
kuwa kwa upande wa Serikali tunasikitishwa na kufadhaishwa sana na tuhuma nzito
kwamba labda waasisi wetu hawakuwa makini au walitufanyia kiini macho.
Hatukutarajia wawepo Watanzania wenzetu, wafikie hapo.
Ni jambo zito. Vile
vile hatukutarajia kuwa Serikali itatuhumiwa kuwa haikuwa makini kuhifadhi
waliosaini waasisi wetu.
Matumaini yetu ni kuwa
baada ya leo tutaendelea na mambo ya msingi kwa mustakabali, umoja na uimara wa
Taifa letu badala ya kuchochea hisia kuwa Muungano wetu hauna msingi imara wa
kisheria.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya
Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
14 Aprili, 2014
No comments:
Post a Comment