Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania Sheikh Ponda Issa Ponda (kulia) akiwa na mshitakiwa mwenzake Saleh Mukadam wakielekea kupanda basi la magereza baada ya hukumu ya kesi yao ya uchochezi kuahirishwa hadi Mei 9, 2013.
Wafuasi Sheikh Ponda wakiwa wamekusanyika nje ya Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo.
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam imeahirisha
kutoa hukumu ya kesi ya uchochezi na wizi wa malighafi zenye thamani ya Sh.
milioni 59 inayomkabili Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu na wenzake 49
kwa maelezo kuwa hakimu aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo,Victoria Nongwa hayupo.
Hakimu Mkazi Alocye
Katemana ndiye aliyeairisha kesi hiyo ambapo alianza kwa kusema kesi hiyo jana
ilikuja kwa ajili ya kutolewa hukumu, lakini hukumu hiyo haitatolewa kwa sababu
hakimu anayesikiliza kesi hiyo hayupo na wala hajatuma hukumu ya kesi hiyo kwa
uongozi wa mahakama.
“Kwa sababu hiyo
naairisha kesi hii hadi Mei 2 itakapokuja kwa ajili ya kutajwa na Mei 9 mwaka
huu, itakuja kwa ajili ya kutolewa hukumu...”
Alisema Hakimu
Katemana na kuamuru mshitakiwa wa kwanza na watano (Ponda na Mukadam Swalehe)
kurudishwa rumande kwa kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Dk Elizer Feleshi
hajaondoa hati yake ya kuwafungia dhamana.
Mwandishi wa habari
hizi ambaye alifika mahakamani hapo tangu saa moja asubuhi, alishuhudia kundi
la watu zaidi ya mia moja wakiwa wamesimama nje ya uzio wa mahakama hiyo karibu
na ofisi ya Maktaba ya
Taifa tayari
wakisubiri kuingia ndani ya lango la mahakama hiyo kwa ajili ya kukaguliwa kwa
vifaa maalum na wanausalama.Watu hao waliruhusiwa kuingia ndani ya viwanja vya
mahakama, lakini ni wachache tu ndiyo walioruhusiwa kuingia ndani ya chumba cha
wazi Na.2 cha mahakama hiyo kwa ajili ya kusikiliza kesi hiyo.
Baada ya kuarishwa
kwa kesi hiyo, askari magreza waliondoka na msafara wa magari yao ambao ulikuwa
ukiongozwa na askari polisi waliokuwa wamevalia na wasiovalia sare za jeshi.
Wakati wakitoka ndani
ya viwanja hivyo tayari kuelekea katika gereza la Segerea anapoishi Ponda na
Mukadam kwa sasa, wafuasi hao walipaza sauti huku wakimpungia mkono Ponda
wakisema ‘Takbir!’ na kuitikia ‘Allahu Akbar.’
No comments:
Post a Comment