Thursday, April 4, 2013

RUKWA: WAJAWAZITO WANG'ATISHWA NGE ILI WAPATE UCHUNGU HARAKA





Wakunga wa jadi mkoani Rukwa, wamekuwa wakitumia nge kusaidia wajawazito waliopitiliza muda wa kujifungua, kupata uchungu na kujifungua salama.Uchunguzi uliofanywa na mwandishi, umebaini kuwa wajawazito wanaokwenda kwa wakunga wa jadi wakiwa na tatizo la kupitiliza muda wa kujifungua, hung’atishwa nge mwilini ili wapate uchungu.

Wakunga waliozungumza na mwandishi kwa masharti ya kutotajwa majina yao, walisifu sumu ya mdudu huyo inayodaiwa kuwa kali, kwa kusababisha mjamzito aliyepitiliza muda, kupata uchungu na kujifungua salama.“Ni sawa na hospitalini, mjamzito unapofika muda wa kujifungua, inaweza kutokea siku zake za kujifungua zimepitiliza na madaktari humpa dawa ya kuongeza uchungu na hatimaye hujifungua.

“Vivyo hivyo nasi tunawang’atisha nge wajawazito, tena hatuwaarifu kuwafanyia hivyo, tunashitukiza na wengi tunaowafanyia hivyo, hujifungua salama,“ alisema mmoja wa wakunga hao wa jadi.
Mmoja wa waliopata kung’atishwa nge, akijitambulisha kwa jina moja la Maria, alikiri kuongezwa uchungu kwa kung’atishwa mdudu huyo mwilini bila kujiandaa kuwa atafanyiwa hivyo, ambapo alidai hatimaye alijifungua mtoto wake wa kiume salama.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa bado ni jambo la busara na salama kwa wajawazito kujifungulia katika vituo vya kutolea huduma ya afya, kuliko kujifungulia kwa wakunga wa jadi, ambao wengi wao hawana ujuzi Wa  kutosha pale mama anapopata matatizo makubwa ya uzazi wakati wa kujifungua.

Maria alidai kuwa wanalazimika kujifungulia kwa wakunga wa jadi hususan vijijini, kutokana na uhaba wa watumishi katika vituo vingi vya kutolea huduma ya afya hususani vijijini, na wakunga wa jadi huwatoza kati ya Sh 10,000 na Sh 15,000.Diwani wa Kata ya Kipili, wilayani Nkasi, Basilio Mbwilo, alikiri wakunga wa jadi kutumia nge kwa wajawazito ili kuwaongeza uchungu wajifungue haraka.

“Hiyo ni kweli kabisa, wala si siri, unajua sumu ya nge ni kali sana, kama ilivyo hospitalini wajawazito wanaopitiliza siku za kujifungua, hupewa dawa ya kuwaongeza uchungu, sasa hiyo ni kitaalamu zaidi.“Basi ni hivyo pia vijijini kwa wakunga wa jadi, ni kweli wanatumia nge kung’atisha wajawazito mwilini.
Sumu ya nge wanaamini kuwa inasaidia kumwongeza mama uchungu wa uzazi kwa kasi ya ajabu, lakini wanawashitukiza hawawataarifu kwanza, si unajua uchungu mtu anaoupata akiumwa na nge?” Alihoji Mbwilo.

Mratibu wa Mradi wa Uhamasishaji wa Afya ya Uzazi Rukwa (TMEP), Dk John Komba, alidai hawezi kusema moja kwa moja kuwa sumu ya nge inaweza kumwongeza mjamzito uchungu wa uzazi, kwani inatakiwa sumu hiyo ifanyiwe utafiti wa kitabibu, ili kubaini kama ni salama kwa matumizi ya binadamu.
“Mimi ningeshauri akina mama wanapobaini kuwa na ujauzito, waanze kuhudhuria na kujifungulia katika vituo vya huduma ya afya kwa ajili ya usalama wao na mtoto atakayezaliwa na si vinginevyo,” alisisitiza Dk Komba.

Muuguzi wa Manispaa ya Sumbawanga, Tizowere Munkondia, alisema haamini kama sumu ya nge, ni njia sahihi kwa sasa, wakati kuna huduma bora inayotolewa kwa wajawazito katika vituo vya kutolea huduma ya afya mkoani humo.
Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni na hali ya kujifungua katika wilaya ya Sumbawanga, kati ya wajawazito 16,581 wilayani humo, 12,483 walijifungulia katika vituo vya huduma ya afya sawa na asilimia 76.3.

Pia takwimu hizo zinaonesha kuwa wajawazito 3,729, walizalishwa na wakunga wa jadi wilayani humo, ambapo 372 walijifungulia njiani.Nge hupendelea kuishi maeneo yenye joto ingawa wapo pia wanaopendelea kuishi katika maeneo yenye ubaridi milimani na katika maeneo ya kawaida. Pia huweza kuonekana majumbani.

Nge wa njano mwenye mikia bapa - Androctonus australis- miili yao ina pingili 18 na kwa kawaida huwa na urefu wa kati ya sentimeta tano na 10, lakini aina nyingine hususan Pandinus imperator huweza kufikia urefu wa kati ya sentimeta 20 na 30.

‘Sindano’ yake anayotumia kung’ata iko mwishoni mwa mkia. Ana vifuko viwili ambavyo hutengeneza na kutunza aina mbalimbali za sumu. Hutumia sindano kwa kazi mbalimbali: kukamata mawindo, kujilinda na hata wakati wa kujamiiana.Nge hufanya kazi zake usiku. Na hula viumbe hai: buibui, wadudu, viluwiluwi na wakati mwingine mijusi na panya wadogo.

Aina zote za nge wana sumu zinazoweza kudhuru hasa wadudu na kuwaua, lakini ni idadi ndogo tu ya nge katika aina zaidi ya 1,050 duniani ndio hatari kwa binadamu.Sumu ya nge ina kemikali nyingi, ambazo hazijachunguzwa. Sumu kutoka nge mmoja inaweza kuwa na kemikali ambazo ni maalumu kudhuru aina fulani ya viumbe.

Nge anapong’ata maumivu yake hudumu kwa saa moja na huweza kusababisha ganzi, mwili kukakamaa na mwasho katika eneo lililong’atwa.Baadaye uchungu unaweza kuenea na kusisimua mwili, kupandisha joto la mwili; uso, ulimi, na kifua huvimba sambamba na maumivu makali kifuani au mgongoni.
Baadhi ya aina za nge (Pandinum imperator, Leiurus quinquestriatus, Buthus occitanus, Androctonus australis, n.k.) wana uwezo wa kudunga kiasi kikubwa cha sumu.

Katika matukio kama hayo, mwathirika hupata homa, hujawa mate kinywani, ngozi humkauka, hupatwa kichefuchefu au kutapika, huchanganyikiwa, huzimia, huku pia mapigo ya moyo yakipungua au kuongezeka, joto la mwili kubadilikabadilika na mapafu kujaa maji na wakati mwingine hutokea moyo au mapafu kushindwa kufanya kazi.

Hata hivyo, uwezekano wa mwathirika kupoteza maisha kutokana na sumu ya nge huwa mdogo kwani hutegemea kiwango cha sumu iliyodungwa na umbile la aliyeng’atwa kwa maana ya ukubwa au udogo wa mwili, lakini pia hali ya kiafya ya aliyeng’atwa; watoto wako hatarini zaidi kuliko watu wazima kutokana na maumbo yao.

No comments:

Post a Comment