Friday, May 30, 2014

JITATHMINI,JICHEKECHE KISHA JIONGEZE




Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Geita Joseph Msukuma.


CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Geita kimemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Geita Bi. Irene Mwakalinga kujipima na kuona kama anatosha kuwatumikia wananchi wa mji huo badala ya kutumia maamuzi ya ubabe na kuwaburuza katika utekelezaji wa majukumu yake.


Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa CCM mkoani humo Joseph Msukuma alipozungumza na waandishi wa habari jana jijini Mwanza, alieleza kuwa, Mkurugenzi Irene Mwakalinga, amekuwa mwanzilishi wa kuibua migogoro kwa maamuzi yake ya kibabe bila kuwahusisha wananchi na badala yake amekuwa akitoa maamuzi kwa kisingizio cha utekelezaji wa sheria za Mipango Miji.

Msukuma alieleza kuwa kufatia uamuzi huo kupingwa na wananchi na kuufikisha kwa viongozi wa CCM Mkoa wa Geita na kuchukua hatua ya kuingilia kati kutaka kufahamu ukweli juu ya jambo hilo kulizua mjadala mkali na kupelekea kuibuka mgogoro kwa muda wa siku 25 baina ya viongozi wa Chama hicho na Mkurugenzi huyo pamoja na Mwenyekiti Halmashauri hiyo.
  
“Hivi karibuni wananchi ambao ni wafanyabiashara wa mji wa Geita waliamuliwa kuondolea  katika soko lililopo katikati mjini humo kutokana na eneo hilo kudaiwa kupewa mwekezaji bila kuwahusisha wananchi jambo lililozua mgogoro baina ya wananchi na mzabuni aliyefika kuanza ujenzi wa choo kwenye eneo hilo, hali iliyopelekea wananchi kulalamika kwa viongozi wa CCM Mkoa huo,”alieleza.

Msukuma alieleza kwamba Mkurugenzi huyo amekuwa na tabia ya kutoa maagizo hayo na kuamuru kuwaondoa wananchi waliokuwa wanafanya shughuli za biashara katika baadhi ya masoko lilikwemo la katikati ya mji huo hali iliyopelekea uongozi wa CCM Mkoa kumuomba Mkuu wa Mgoa wa Geita Said Magalula kuitisha kikao cha pamoja kushirikisha wadau wote.

“Mkuu wa Mkoa Magalula alikubaliana na ombi la Chama na jana aliitisha kikao hicho ambacho kiliwashirikisha viongozi wa Halmashauri, CCM Mkoa na Wilaya, wananchi ambao ni wafanyabiashara wa soko hilo ili kujaribu kubaini ukweli iwapo taratibu zilifuatwa na wananchi kuhusishwa juu ya ujenzi huo ikiwa pia kupewa eneo mbadala la kufanyia shughuli zao,” alisema.

Kwa mujibu wa Msukuma wakati wa kikao hicho maelezo kutoka pande mbili kati ya Halmashauri na wananchi zilisikilizwa kwa umakini na Mkuu wa Mkoa na wajumbe wa Kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa huo, ambapo wananchi walikubali kuupokea mradi huo lakini unatekelezwa eneo gani ndipo kuliibua hoja ya malalamiko kutoka kwa wananchi.

Alieleza kuwa baada ya kelele za malalamiko ya wananchi huku majibu yaliyotolewa na Mkurugenzi huyo yakionekana kutojitosheleza hali iliyobainika kukiukwa kwa utaratibu mzima ikiwa ni pamoja na utolewaji wa zabuni hiyo jambo ambalo, Mkuu wa mkoa alifikia uamuzi wa kutoa amri ya kusitishwa haraka kwa ujenzi wa mradi huo unataraji kugharimu Sh. Milioni 90.

“Tulikubaliana kwa pamoja kuwa choo hicho sasa kijengwe eneo la awali lilipo jengo la zamani linalo milikiwa na halmashauri, tumeafikiana na wadau wote kwenye kikao hicho, tunataraji maamuzi na maagizo ya serikali ya mkoa yatafuatwa na kuwa mwisho wa mgogoro huo, kwa hili nampongeza sana Magalula na Kamati yake pamoja na wananchi kuwa waelewa,”alisema.

"Hebu pima hili Mkurugenzi mama Mwakalinga alianzisha tozo ambazo hazikuzingatia sheria, tozo ambazo hazikusainiwa na Waziri Mkuu, tozo zilizokuwa za aina yake kwa kuamrisha Misikiti, Makanisa, Shule kulipa tozo na kweli zilitekeleza na ushahidi tunao tulimpa hadi Waziri Mkuu, kama wadau hao wakirudi nyuma na kudai fedha zao hasara kwa nani? sasa ajitathimini kwa hayo kama anatosha basi aendelee na utekelezaji lakini kama hatoshi basi ajiweke kando kupisha wengine"

Aidha Msukuma amedai kuwa mnamo Mwaka 2012 Mkurugenzi huyo alitengeneza mitaro ile hali akijua kuwa barabara husika litakwenda kufanyiwa matengenezo makubwa hivyo itavunjwa, mitaro hiyo iliyogharimu zaidi ya milioni 115 ilipo kamilika tu baada ya mwezi mmoja ilivunjwa na serikali ikaingia hasara.

Mwenyekiti huyo ameongeza kuwa mara kadhaa kupitia vikao mbalimbali wamekuwa wakimshauri Mkurugenzi huyo kuwa masuala yote ya maamuzi yanayohusu wananchi lazima akutane na wananchi wachangie maoni yao na wampe ushauri badala ya kukaa tu mezani bila utafiti na kutoa tamko.

"Ninadiriki kumwita mzigo kwa sababu moja, Mweshimiwa Waziri wa TAMISEMI alipokuja wananchi walimuonyesha eneo la Stendi, stendi ile ili chakachuliwa na waziri alitoa siku sitini iwe imerekebishwa lasivyo atakuja kumrekebisha yeye, alichokifanya nikurundika udongo ambao uko mpaka leo, sasa kama yeye hawezi tunaendeleaje sisi wanasiasa kuvumilia kuona Mawaziri wetu wakiitwa mizigo wakati mizigo tunayo huku" alisema Msukuma na kuongeza kwa kusema.  
"Sasa sisi wawakilishi wa chama wasaidizi wa Mawaziri, wasaidizi wa Rais tunasema wale wote watakaojitathimini na kujiona kuwa mizigo kwa halmashauri zetu wajitathimini na kutafuta sehemu nyigine za kwenda"

Hata hivyo Clouds Fm ilipojaribu kumtafuta kwa njia ya simu mkurugenzi huyo kuzungumzia suala hilo na kupata uamuzi wa kiongozi huyo simu iliita pasipo kupokelewa.

No comments:

Post a Comment