Monday, May 26, 2014

TAARIFA






TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Mkutano wa Tatu wa Mwaka wa Kitaifa wa Mashauriano Kati ya MCT na Wahariri kufanyika Kilimanjaro
Baraza la Habari Tanzania (MCT) litafanya mkutano wake wa tatu wa mwaka wa Mashauriano na Wahariri huko Machame, mkoani Kilimanjaro kuanzia Mei 29 hadi 30 mwaka huu. Mkutano huo utafunguliwa rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mheshimiwa Leonidas Gama.


Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga amesema huu utakuwa ni mkutano wa tatu wa aina hii kufanyika hapa nchini, ambapo wahariri wapatao 52 kutoka nchini kote watahudhuria.

Alisema mkutano huo umeandaliwa mahususi kuliwezesha Baraza na Wahariri ambao ni watendaji muhimu katika vyombo vya habari, kukutana na kujadiliana masuala muhimu yanayohusiana na taaluma na changamoto ambazo vyombo vya habari vinakutana nazo, na hivyo kutafuta njia ya kuzipatia ufumbuzi.

Kauli mbiu ya mwaka huu inasema: “Kuimarisha Weledi na Maadili ya Uandishi wa Habari.” Katika mkutano huo, Baraza la Habari na Wahariri wataweza kutathimini na kuangalia changamoto ambazo zilijitokeza toka mkutano wa pili ulipofanyika.

Mada mbali mbali zinazotarajiwa kujadiliwa katika mkutano huo ni pamoja na Ripoti ya Ufuatiliaji wa Vyombo vya Habari ya mwaka 2013, changamoto ambazo wahariri wanakutana nazo kwenye vyumba vya habari na Rasimu ya pili ya Katiba mpya, Ibara ya 30 na 31.

Wahariri hao pia watajadiliana juu ya masuala mengine muhimu ikiwemo jukumu la vyombo vya habari katika uchaguzi mkuu ujao na changamoto zake, ripoti ya majaji wa EJAT 2013, pamoja na ushirikiano kati ya vyombo vya habari na serikali.

Mkutano wa pili wa mashauriano kati ya MCT na Wahariri ulifanyika mwaka jana mwezi Mei mjini Tanga na kuhudhuriwa na wahariri 45.


Kajubi D. Mukajanga
Katibu Mtendaji
Mei 23, 2014

No comments:

Post a Comment