Friday, May 9, 2014

NAIROBI KUFUNGUA KITENGO KIPYA CHA ASKARI POLISI WANAOVAA VIATU VYA MAGURUDUMU




 
Wakati akitembea kandokando ya barabara ya Kenyatta katika wilaya ya biashara ya katikati ya Nairobi wiki iliyopita, Ann Wanjiru, mwenye umri wa miaka 27, alivamiwa na vijana wa kiume watatu waliodai kupotea na kuhitaji kuelekezwa.

Polisi wa utawala wa Kenya wamepewa mafunzo ya kutumia viatu vya magurudumu kuonyesha ujuzi wao tarehe 17 Aprili katika kambi ya mafunzo ya Embakasi.

Wakati aliposimama kuwasaidia, wanaume hao walimzunguka kwa namna waliyompigia mahesabu: mmoja wao alimchomolea kwenye mfuko wake wa mkononi, mwingine alimkapua hereni na mkufu, wakati wa tatu alimvuruga, akifanya naye mazungumzo.

"Tukio hilo lilichukua muda wa chini ya dakika moja," alisema Wanjiru, ambaye anaendesha mgahawa wa chakula katika barabara ya River huko Nairobi. "Wakati wanaume hao walipochukua kwa nguvu niling'amua kwamba walikuwa waporaji. Nilijaribu kutoa sauti ya kuomba msaada lakini nilikuwa nimechelewa kwani tayari walikuwa wameshatokomea kwenye msongamano wa watu."

"Nilikuwa nikisikia visa hivyo, lakini hii ilikuwa mara yangu ya kwanza kukutana na waporaji," aliiambia Sabahi, akiongezea kwamba alipoteza shilingi 20,000 (dola 230) ambazo alikuwa amebeba kulipia ada ya kijana wake wa kiume.

"Somo nililojifunza ni kwamba sitasimama kusaidia au kumsikiliza yeyote anayedai kukwama," alisema. "Ni bahati mbaya kwamba hata kwa watu ambao kweli wanahitaji msaada wanaweza kuachwa wenyewe [pasipo kusaidiwa], lakini wakaazi hawawezi kulaumiwa kwa kuwa na ukatili huu."

"Jiji hili limetulazimisha kwa hili," alisema.Uporaji umeibuka

Kamanda wa polisi wa Nairobi Benson Kibue alisema uporaji, ikiwa ni pamoja na wezi wa mifukoni na magenge mabaya ya barabarani, wameibuka katika jiji hili.

"Hakuna siku inayopita pasipo matukio kama hayo kuletwa katika vituo vyetu vya polisi," alisema. "na kinachotia wasiwasi zaidi ni kwamba hali hiyo inaongezeka."

Kibue alisema waporaji na wezi wa mifukoni wanatumia mianya ya mitaa yenye msongamano wa watu na barabara zenye msongamano katika jiji hili, wakijua kwamba hawawezi kukamatwa kwa urahisi.

Lakini polisi wanaamini hali hii itabadilika kuanzia tarehe 1 Julai, wakati timu mpya ya maofisa wa polisi watakaokuwa wakitumia viatu vyenye magurudumu watasambaa katika mitaa ya Nairobi.

Maofisa arobaini kutoka katika Uongozi wa Polisi wanapata mafunzo ya kutumia viatu vya magurudumu, alisema Kibue, na baada ya kumaliza watatumika katika mitaa mikubwa katika mji mkuu pamoja na maeneo ya makazi ya jiji.

Alisema majaribio ya awali ya kukabiliana na uhalifu yaliyofanywa na maofisa kwa kutumia pikipiki hayakuwa na ufanisi kwa sababu mitaa iliyo na msongamano ilizuia wao kupita. Alieleza kuwa na matarajio mazuri zaidi kuhusu jitihada mpya za kutumia viatu vipya vya magurudumu.

"Tuna uhakika kwamba mbinu hii ya kisasa itafanya kazi kwa sababu haiko kama jitihada zile za awali, polisi wanapotumia viatu vyenye magurudumu watazunguka jiji kwa urahisi," aliiambia Sabahi. "Mizunguko kwa kutumia magari ya doria na pikipiki imekuwa migumu na hata polisi walio kwa miguu wamekuwa hawana uwezo wa kuwakamata wezi ambao wanakimbia kwa haraka katika operesheni zao."

Alisema wazo la kutoa mafunzo kwa polisi kuhusu kutumia viatu vya magurudumu lilianzia miezi mingi kwa utafiti na mipango na linahitaji kuongeza uwezo wa polisi kushughulikia matukio ya uhalifu yanayoibuka.

"Zaidi ya [maofisa katika] viatu vya magurudumu, jiji pia litasambaza matumizi ya mbwa wa kunusa ili kuwasaidia maofisa kuchunguza vituo vya mabasi," alisema. "Mikakati hii itatumika kwa pamoja hadi mitaa itakapokuwa huru dhidi ya uhalifu."

Kibue alisema Nairobi ilichaguliwa kufanyiwa majaribio ya programu hii kwa sababu ya kuongezeka kwa matukio ya uporaji, lakini kutegemea na mafanikio ya programu, inaweza kusambazwa katika siku zijazo hadi Mombasa na Kisumu.

Wanjiru, mwathirika wa uporaji katika Mtaa wa Kenyatta, alipongeza jitihada mpya za polisi, akisema linaweza kuwa ndiyo suluhisho lililokuwa likihitajika katika uhalifu unaojitokeza ovyo jijini.

Alisema kama timu ingekuwa imeanza operesheni wakati alipoporwa wiki iliyopita, labda wahalifu wangekamatwa na vitu vyake vingerejeshwa.

Kwa Julius Omondi, mwenye umri wa miaka 40, muuzaji wa bima jijini Nairobi, jitihada hizo zimekuja kwa kuchelewa kidogo.

Omondi alisema ameshaporwa mara mbili katika miezi sita iliyopita, uporaji wa mara ya mwisho ulitokea tarehe 20 Aprili wakati akiendesha gari katika Mtaa wa Moi, ambapo alishusha vioo vya gari lake baada ya mtu kumsogelea na kumwonyesha ishara za kuwa tairi lake lilikuwa na pancha kubwa.

"Katika punde nilisikia milango ya nyuma ya gari ikifunguliwa kwa nguvu na kuona laptop yangu ambayo ilikuwakwenye kiti cha nyuma ikivutwa nje," aliiambia Sabahi. "Nilipiga kelele na Wasamaria wema waliokuwa mtaani walijaribu kuwafuata wezi, lakini hawakuweza kufanikiwa kuwakamata, na hivyo ndivyo nilivyopoteza laptop yangu."

"Sasa, ninawapuuza watembea kwa miguu wote wanaojaribu kunipoteza mawazo," alisema.
Viatu vya magurudumu 'badiliko la mchezo' kwa kuzuia uhalifu barabarani

Joel Andanje Obanda, mkurugenzi wa mafunzo ya mwendo wa kasi katika Shirikisho la Kenya la Kuteleza kwa Rola, alisema kuwasambaza polisi katika ukimbiaji kwa viatu vya magurudumu kutatoa msukumo kwa jitihada za kupambana na uhalifu.

"Polisi walio katika viatu vya magurudumu wataweza kutumia ujanja kwa urahisi katika mitaa yetu yenye watu wengi na watakuwa na haraka [kuliko maofisa wanaotembea], hivyo kuwafukuza wahalifu na kuwakamata kwa sasa itakuwa ni halali," aliiambia Sabahi.

Alisema miji mikubwa duniani kote kama vile Berlin, Jakarta na Dubai imeonyesha mafanikio katika kuwatumia maofisa wa polisi katika utumiaji wa viatu vya magurudumu ili kukamata ukiukaji wa usalama barabarani na wakosaji wengine wadogowadogo.

Lakini Jared Kutswa, mwenye umri wa miaka 32, fundi ya mekanika katika eneo la viwanda Nairobi ambaye alisema pia amewahi kuibiwa mara mbili, alionyesha wasiwasi kwamba timu ya polisi itakuwa na uwezo wa kuzuia wahalifu ambao wamezidi katika mitaa ya mji mkuu.

"Sina imani na jitihada za serikali katika kuwaondoa wezi katika mitaa," alisema. "Elimu kidogo niliyonayo kuhusu viatu vya magurudumu ni kwamba vinaweza kuwa tu na manufaa pale ambapo barabara ni za lami, sio katika mashimo au uchafu."

"Pia, nina hofu kwamba wahalifu wanaweza kutumia viatu vya magurudumu, wakiwashinda polisi katika mchezo wao wenyewe," alisema.

Hata hivyo, Obanda alipuuza wasiwasi huo akisema viatu vya magurudumu vinaweza kutumika kwenye majani na hata ardhi isiyonyooka, pamoja na katika njia ya waendao kwa miguu.

"Yote inategemea mafunzo," alisema. "Ukimbiaji kwa viatu vya magurudumu [katika njia] unaweza kutumika katika aina zote za ardhi na tunaamini ni ubadilishaji wa mchezo halimuradi tu uzuwiaji uhalifu katika mitaa yetu unahusika."

No comments:

Post a Comment