Wednesday, February 26, 2014

MSWADA WA SHERIA UNAOPINGA MAPENZI YA JINSI MOJA UMEKUWA SHERIA NCHINI UGANDA




Rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni, akiwa eneo la Rwakitura karibu na mji wa Kampala, septemba 24 mwaka 2012
 

Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni, ametia saini leo jumatatu kwenye sheria inayopinga ndoa ya watu wa jinsia moja, ambayo awali, alikataa kutia saini, akihofia kwamba nchi yake itatengwa na wafadhili wake, mkiwemo Marekani, ambayo hivi karibuni, rais wa nchi hio, Barack Obama, alimuonya rais Museveni kutotia saini kwenye sheria hio.Hayo yamethibitishwa na msemaji wa ikulu.

Mswada huo wa sheria uliyoidhinishwa katikati mwa mwezi wa desemba, unapinga mapenzi ya watu wa jinsi moja, na kuwalazimu watu kunyooshea kidole yeyote anaejihusisha na kitendo hicho.

Mswada huo ambao sasa utakuwa sheria, unatoa adhabu ya kifungo cha miaka 14 jela kwa wale watakaopatikana na hatia kwa mara ya kwanza

Vifungo vya sheria vilivyozua utata, ambavyo vinatoa adhabu ya kifo kwa watu watakaorudi kushiriki kitendo cha watu wa jinsia moja, au mtu yeyote ambaye atapatikana ameshiriki kitendo hicho na mtoto wa kiume alie na umri uliyo chini ya miaka 18, au anajitambua kwamba ameathirika na ukimwi, vifungo hivyo vilifutwa, lakini sheria hio bado inaendelea kukosolewa na wanaharakati wa haki za binadamu na mataifa ya magharibi.

Mapema leo asubuhi, msemaji wa ikulu,Tamale Mirundi, amethibitisha kwamba rais atatia saini leo kwenye mswada huo ili uwe sheria, ambayo itaanza kutekelezwa, baada ya saini hio.

“Rais atatia saini leo kwenye sheria inayopinga mapenzi ya watu wa jinsia moja”, ameimbia AFP, msemaji wa ikulu, Tamale Mirundi, akibaini kwamba rais Museveni hawezi kupewa shinikizo na mataifa ya kigeni.

Tamale Mirundi, amesema sheria hio itatiliwa saini kwa faida ya Uganda, na si kwa faida ya mataifa ya kigeni, akibaini kwamba “Uganda ni taifa linalojitawala, na sheria zake zinapaswa kuheshiwa”.

Mshindi wa tuzo ya Nobel na raia wa Afrika Kusini, mchungaji Desmond Tutu amemuonya rais wa Uganda Yoweri Museveni dhidi ya kutia saini sheria tata inayokataza ndoa za jinsia moja akitolea mfano harakati zilizokuwa zikifanywa na utawala wa Kinazi wakati wa ubaguzi wa rangi walipotunga sheria kuzuia watu kupendana.

Mchungaji Tutu, ameeleza kushtushwa na namna ambavyo suala hilo linachukuliwa nchini Uganda na kuongeza kuwa yeye angeona nchi hiyo itunge sheria kudhibiti watu wanaotekeleza vitendo vya ubakaji, unyanyasaji wa watoto na biashara ya ngono badala ya kutia saini sheria inayokataza ndoa za jinsia moja.

Kiongozi huyo amekosoa majibu ya kisayansi yaliyotolewa na jopo lililochunguza sababu za watu kuwa mashoga na kumshauri rais Museveni kutia saini badala yake amesema mtu kuwa shoga ni asili ya mabadiliko ya binadamu na sio shida.

Ameongeza kuwa kupitishwa kwa sheria hiyo inayopiga marufuku ndoa za watu wa jinsia moja kunarejesha utawala wa zamani wa kikoloni ambao ulikuwa unaharakisha kupitisha sheria zinazokataza watu kupendana.

No comments:

Post a Comment