Mratibu wa Mbio za Uhuru Marathon, Innocent Melleck
akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo wakati akizungumzia
maandalizi ya uzinduzi wa Mbio hizo kwa Mwaka 2014,ambapo mwaka huu Mbio hizo
zitazinduliwa kwenye Kijiji cha Butiama,Mkoani Mara.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Selemani
Nyambui akinzungumza kwenye Mkutano huo.
MBIO za Uhuru (Uhuru Marathon) zinatarajiwa kuzinduliwa rasmi
katika kijiji cha Butiama mkoani Mara, Agosti mwaka huu, huku lengo kubwa likiwa
ni kudumisha amani, umoja na mshikamano miongoni mwa Watanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana,
Mratibu wa Uhuru Marathon, Innocent Melleck alisema, wameamua kuzindulia
Butiama ili kumuenzi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ambaye katika uhai
wake alipigania mno mambo hayo.
“Tukumbuke Mwalimu Nyerere alipigania mno amani, umoja na
mshikamano miongoni mwetu, pia ndiye muasisi wa Taifa hili, hivyo tuliona bora
tukazindulie Butiama ili kumuenzi.”
Alisema, mara baada ya uzinduzi huo wanatarajia kuzunguka nchi
nzima kuanzia ngazi ya wilaya, ili kuzitambulisha mbio hizo na kuwakumbusha
Watanzania umuhimu wa amani, umoja na mshikamano miongoni mwetu.
Melleck alisema, kiini cha kuanza kampeni ya kuzindua mbio hizo
mapema imekuja, kwani zenyewe zimebeba ujumbe wa amani, umoja na mshikamano,
hivyo ni vyema kuwakumbusha Watanzania umuhimu wa kutunza na kuenzi mambo hayo.
“Amani ya nchi yetu katika siku za hivi karibuni inaonekana
kwenda vibaya hasa kutokana na baadhi ya vyama vya siasa kufanya siasa kwa
visasi badala ya kujenga hoja kukabiliana na changamoto za kisiasa, hivyo ni
jukumu letu kuilinda,” alisema.
Naye Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Selemani
Nyambui alisema, kuanza maandalizi mapema kwa mbio hizo ni faraja kwao na
watahakikisha wanakabiliana na changamoto zote ili ziweze kufana.
Mbio hizo zinatarajiwa kufanyika Desemba 8, mwaka huu na kwa
mara ya kwanza zilifanyika mwishoni mwa mwaka jana na kushirikisha wanariadha
kutoka nchi mbalimbali.
No comments:
Post a Comment