Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mheshimiwa
Jakaya Mrisho Kikwete(Pichani)
amesema kuwa kampeni za kugombea kuteuliwa kuwa
mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) hazijaanza rasmi.
Aidha, Rais Kikwete
amesema kuwa vitendo vya baadhi ya watu kuanza kampeni kabla ya wakati wake ni
moja ya mambo yanayosikitisha.
Hata hivyo, Rais
Kikwete amesema kuwa suala hilo zima limekabidhiwa kwa Makamu wa Mwenyekiti wa
CCM (Tanzania Bara) Mzee Philip Mangula ambaye atalisimamia jambo hilo na
kulishughulikia.
“Kuhusu kama kampeni za
kuwania Urais zimeanza ni kwamba kampeni hazijaanza rasmi. Hili ni moja ya
mambo yanayosikitisha. Lakini suala zima tumelikabidhi kwa Mzee Mangula ambaye
atalisimamia na kulishughulikia,” Rais Kikwete alisema, Februari Mosi, 2014.
Rais na Mwenyekiti wa
CCM alikuwa anazunguza na wajumbe wa Halmashauri ya CCM ya Mkoa wa Mbeya kwenye
Ukumbi wa CCM mjini Mbeya. Rais Kikwete yuko katika ziara ya kikazi ya siku
mbili mkoani Mbeya.
Rais Kikwete
alilizungumzia suala hilo baada ya kuwa ameulizwa moja kwa moja na Mwenyekiti
wa CCM wa Mkoa wa Mbeya, Ndugu Godfrey Zambi ambaye alimtaka Mheshimiwa Rais na
Mwenyekiti wa chama chake kufafanua kama kampeni zimeanza ama bado.
No comments:
Post a Comment