Kamanda Geofrey
Kamwela
Watu wawili akiwemo
mtoto wa miezi sita wamekufa na wengine 40 kujeruhiwa katika ajali ya
barabarani, iliyolihusisha basi la Zuberi katika eneo la Tumaini Nkuhi kwenye
barabara kuu ya Singida – Dodoma. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida, Geofrey
Kamwela alisema mjini hapa kuwa ajali
hiyo ilitokea jana saa 7:15 mchana na ilihusisha gari la abiria la
Zuberi, lenye namba za usajili T.119 AZZ Scania.
Alitaja waliokufa kuwa
ni Sivilari Aloyce “Logotio” ( miezi 6) na mwanamke mmoja mtu mzima aliyepandia
Shinyanga, ambaye jina lake halikuweza kupatikana. Alisema miili yao
imehifadhiwa
hospitali ya mkoa
ikisubiri ndugu zao. Akieleza ajali ilivyotokea, Kamwela alisema basi hilo lilikuwa
linatoka Mwanza kwenda Dar es Salaam na lilipofika sehemu hiyo, alitokea mtu
mmoja barabarani ambaye alikuwa anayumba, kiasi cha kumbabaisha dereva Fadhili Kalembo.“Katika
juhudi za kumkwepa
mwenda kwa miguu huyo,
basi lilipoteza mwelekeo kasha kupinduka na kusababisha vifo vya watu wawili na
majeruhi” alisema Kamanda.
Alisema baada ya ajali
hiyo kutokea, mwenda kwa miguu huyo alitokomea kusikojulikana. Mganga Mfawidhi
wa Hospitali ya Mkoa wa Singida, Dk Deogratius Banuba alisema majeruhi wanne
wamepewa rufaa kwenda Hospitali ya KCMC Moshi, kutokana na hali zao kuwa mbaya.
Alisema wengine 36 wanaendelea kupatiwa matibabu hospitalini hapo.
Hii ni ajali ya pili kutokea
kwenye eneo hilo katika kipindi kisichozidi wiki mbili. Januari 19, mwaka huu
watu 13 walikufa papo hapo, baada ya gari aina ya Noah, kugongana uso kwa uso
la lori la mizigo
kwenye eneo la Isuna.
No comments:
Post a Comment