Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza na Mkuu wa jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali Said Mwema, ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.
Mohammed Gharib Bilal amekutana na Mkuu wa jeshi la Polisi Inspekta Jenerali
Said Mwema ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam , Jumatatu Mei 27, 2013.
Katika mkutano huo, Mheshimiwa Makamu wa Rais ametumia
nafasi hiyo kumpa pole Mkuu wa Polisi kufuatia ajali ya gari la iliyosababisha
vifo vya askari wanne wa Jeshi hilo, waliokuwa njiani kutoka Nachingwea
kuelekea Mkoani Mtwara kwa kazi maalum ya kudhibiti vurugu zilizojitokeza
Mkoani humo juma lililopita.
Mheshimiwa Makamu wa Rais alisema, askari hao watazidi
kukumbukwa kwa kuwa walikuwa mstari wa mbele kuhakikisha majukumu yao kwa Taifa
hili yanafanikiwa. Mheshimiwa Makamu wa Rais alisema pia kuwa, serikali
inathamini sana mchango wa Jeshi la Polisi sambamba na majeshi mengine kutokana
na kufanya kazi kwa kujitolea na kwa kutambua kuwa ulinzi na usalama wa Taifa
ni jambo muhimu kwa maendeleo ya nchi.
Mheshimiwa Makamu wa Rais alimueleza Mkuu wa Polisi kuwa,
kazi inayofanywa na jeshi lake ni kubwa na kwamba Watanzania wanaithamini sana.
Pia aliongeza kuwa katika nchi zote wananchi wanaojitolea kufanya kazi katika
vyombo vya usalama, ni miongoni mwa wazalendo wakubwa wanaopaswa kuenziwa kwa
kuwa wamekubali kuweka maisha yao kwa ajili ya nchi na watu wake.
Katika mkutano huo, Makamu wa Rais alitumia nafasi hiyo
kupata taarifa kuhusu hali ya usalama mkoani Mtwara na pia kubadilishana mawazo
kuhusu kuhakikisha maeneo ya nchi yetu kubakia salama wakati wote.
Imetolewa na Boniphace Makene
Mwandishi
wa Habari wa Makamu wa Rais
No comments:
Post a Comment