Msemaji wa JWTZ, Kanali Kapambala Mgawe
Dar es Salaam. Tanzania imesema vitisho vinavyoendelea
kutolewa na waasi wa M23 wanaopigana Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya
Congo (DRC), haviinyimi usingizi.
Hata hivyo, imetaka Jumuiya ya Kimataifa kutopuuza vitisho
hivyo.Kauli ya Tanzania inakuja huku kukiripotiwa kuwapo kwa mapigano makali
baina ya vikosi vya Serikali waliopambana na waasi hao, ambao wameanzisha tena
harakati ya kuliteka Jimbo la Goma na maeneo mengine ya jirani.
Mapigano hayo ni ya kwanza tangu M23, kuondoka mjini humo
mwaka jana kufuatia shinikizo za kidiplomasia.Umoja wa Mataifa (UN), umesema
utaongeza kasi ya juhudi zake za kutafuta amani kwa kutuma kikosi cha wanajeshi
3,000 kujaribu kuzima mapigano hayo, ambayo yalisababisha watu 19 kuuawa na
wengine kujeruhiwa.
Msemaji wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Kanali
Kapambala Mgawe alisema vikosi vya Tanzania vilivyoko Congo vitaendelea
kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia weledi na miongozo ya UN.Kanali Mgawe
alisema kauli zozote za vitisho vinazoendelea kutolewa na waasi hao, haziwezi
kurudisha nyuma juhudi hizo.
Hata hivyo, Kanali Mgawe aliitaka Jumuiya ya Kimataifa
kutopuuzia vitisho hivyo“Inawezekana kuna jambo hapa maana kwa nini Tanzania
ipewe vitisho ilhali operesheni hiyo ya amani inahusisha mataifa mengine?”
alihoji Kanali Mgawe.
Nchi nyingine ambazo zimekubali kutuma wanajeshi wake
kupigana na waasi hao ni Malawi na Afrika Kusini.Waasi wa M23 wamekuwa wakitoa
vitisho kwa wanajeshi wa Tanzania, lakini Serikali imekuwa ikitamba kuwa hivyo
ni vitisho na kazi ya kulinda amani itaendelea kama ilivyopangwa. Tayari,
Katibu Mkuu wa UN, Ban-Ki Moon ametembelea nchi hiyo.
Chanzo: mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment