Tuesday, August 6, 2013

SOGA KIDOGO!







kwa wale waliowahi kuwa mashabiki wa soka enzi za miaka ya tisini watamkumbuka nyota wa zamani wa timu ya taifa ya ghana nii ordartey lamptey .

mchezaji aliyeibuka ghafla na kuuteka ulimwengu wa soka akiwa na umri mdogo aliyetabiriwa makubwa ambayo kwa bahati mbaya hayakuwahi kutimia .

hadithi ya lamptey imekuwa ikitumika kuwapa funzo muhimu wachezaji wanaochipukia ambao huweza kujazwa na presha za mashabiki na vyombo vya habari , presha ambayo wakati mwingine ikizidi huharibu badala ya kujenga.
hadithi ya lamptey ilianzia  mwezi disemba mwaka 1974 huko tema nchini ghana ambako alizaliwa .

maisha ya utotoni hayakuwa mazuri kwa lamptey hata kidogo , baba yake ambaye alikuwa muumini wa kilevi alikuwa akimnyanyasa na makovu yaliyoko kwenye uso wa lamptey mpaka hii leo ni mfano wa mateso aliyokuwa akiyapata toka kwa mzee lamptey ambaye alikuwa akizima sigara kwenye uso wa mwanaye.

mara nyingi lamptey alikuwa halali nyumbani akikimbia bugudha ya kero za ulevi wa baba yake mzazi na mambo yalikwenda mrama zaidi wakati wazazi wake walipoachana akiwa na umri wa miaka nane . baba yake wa kambo hakuona sababu ya kuwa naye nyumbani kwake na alimfukuza .

faraja pekee kwa lamptey ilitoka kwenye mchezo ambao alikuwa akiupenda , mchezo wa soka ambao pamoja na matusi na kashfa toka kwa baba yake nii hakuwahi kuachana nao .
kwa bahati nzuri lamptey alijiunga na kambi moja ya kiislamu ambayo ilikuwa 

ikijishughulisha na ukuzaji wa vipaji na hapa angalau mwangaza ulianza kuonekana .
mpaka anafikia umri wa miaka kumi na tano lamptey tayari alianza kuwa nyota na aliitwa kwenye timu za vijana za ghana akianza kwenye timu ya under 17 na mwaka mmoja baadaye akiweka historia ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo kuichezea timu ya taifa ya wakubwa akiwa na umri wa miaka 16 . katika mchezo huo dhidi ya togo lamptey alifunga bao jambo ambalo lilizidi kuwafanya watu wamfuatilie kwa karibu

kabla ya hapo nii aliiteka dunia kwenye michuano ya dunia ya vijana mwaka 89 na mwaka 91 ambapo alitwaa tuzo ya mchezaji bora katika mashindano yaliyowatoa nyota kama juan sebastian veron na marcelo galardo pamoja na alesandro del piero .

timu ya anderletch ya ubelgiji ilimuona nii na kuamua kumsajili wakati huo huo na hapa alipachikwa jina la pele mpya . ubora wa nii ulilazimu hadi sheria zilizozuia vijana walio na umri chini ya miaka kumi nane kubadilishwa ili mradi apate nafasi ya kucheza.

miaka miwili baadaye timu ya uholanzi ya psv ilimuona na kumnunua na baada ya muda mfupi aliuzwa kwenda aston villa . hapa matatizo yalianza kujitokeza ambapo iligundulika kuwa wakala wa nii mtaliano antonio caliendo alikuwa mhuni ambaye alimsainisha mkataba wa kinyonyaji ulioshuhudia wakala huyu akipata fedha nyingi kwa kumuuza nyota huyu .

lamptey hakukaa sana aston villa na baada ya mwaka mmoja tu alijikuta akiuzwa kwenda coventry city ambako hakukuwa tofauti na villa. lamptey aliuzwa nchini italia kwenye klabu ya venezia . hapa majanga yaliendelea ambapo mtoto wake diego alifariki dunia na kumfanya nii kukumbwa na msongo wa mawazo ulimfanya ajiweke kando na mchezo wa soka kwa muda .

baada ya kupata wakala mpya ambaye alikuwa mjerumani lamptey alijaribu bahati yake nchini humo akiwa na timu ya greuther furth . hali ya ujerumani ilikuwa mbaya pengine kuliko mahali kwingine kote alikopita . hapa alikutana na matatizo ya kushindwa kuhimili utamaduni mpya , mtindo wa uchezaji uliohitaji nguvu kupindukia ulimshinda na mbaya zaidi ubaguzi wa rangi kwenye timu yake mwenyewe ambapo kuna kipindi mchezaji 

mwenzie aligoma kulala naye chumba kimoja hotelini eti tu kwa sababu yeye ni mweusi .pigo jingine lilikuja baada ya mtoto mwingine lisa kufariki dunia siku chache baada ya kuzaliwa.

baada ya hapo lamptey alicheza soka nchini china na uarabuni kabla ya kurudi kwao ghana kwenye klabu ya asante kotoko na timu yake ya mwisho ilikuwa jomo cosmos ya afrika kusini.

nii lamptey alikuwa mhanga wa kuharakisha kipaji ambacho hakikuwa tayari , presha kubwa ya mahitaji ya timu ambazo hazikuwa tayari kumpa muda wa kuzoea mazingira , kujifunza kupitia changamoto za maisha mapya ilikuwa kubwa sana na kwa umri wake ilimshinda.

hii leo nii anamiliki shule nyumbani kwao ghana ,shule ambayo lengo lake ni kuwapa furaha watoto akichagizwa na kumbukumbu ya watoto wake wawili ambao ni marehemu diego na lisa.
bado anajihusisha na mchezo wa soka akiwa kama kocha msaidizi wa timu ya sekondi wise fighters .

No comments:

Post a Comment