Sunday, October 28, 2012

UGONJWA WA MARBUG UBAUA KWA ASILIMIA 70-90

Hapa ni nchini Uganda wataalamu wa Afya wakinyunyiza dawa mahali ambapo wagonjwa wa Marbug walitelekezwa hadi kufa, baada ya kugundulika wana ugonjwa huo.

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA AFYA NA USTAWI WA JAMII


 

 

 

 

TAARIFA KWA UMMA.

TAHADHARI YA UGONJWA WA MARBURG
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, imepokea taarifa kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), tarehe 20 Oktoba, 2012 kuhusu ugonjwa wa Marburg ambao umejitokeza katika nchi jirani ya Uganda. Maeneo yaliyokumbwa na ugonjwa huo ni Wilaya ya Kabale, Kanda ya Kusini Magharibi ya nchi, na wilaya hii inapakana na Rwanda. Mpaka tarehe 24 Oktoba 2012, takriban watu 13 wamepata maambukizo na 6 wamepoteza maisha..

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inapenda kutoa tahadhari ya Ugonjwa huu kwa wananchi wote, katika mikoa yote ya Tanzania na hasa wale waliopo katika mikoa ambayo inapakana na na nchi jirani ya Uganda (Mikoa ya Mara, Mwanza, Kagera na Kigoma).

Marburg ni ugonjwa wa hatari unaofanana na Ebola na unasababishwa na virusi vijulikanavyo kwa lugha ya kitaalam “Marburg Virus”. Ugonjwa huu ni miongoni mwa magonjwa yajulikanayo kwa ujumla kama Homa za Virusi zinazosababisha kutokwa damu mwilini, (Viral Haemorrhagic Fevers). Chanzo kamili cha virusi vya ugonjwa huu haki­julikani. Hali inayosababisha mlipuko wake pia haijulikani. Ugonjwa huu hauna tiba wala chanjo.
Dalili kuu za ugonjwa huu ni pamoja na Homa kali, inayoambatana na kutokwa damu katika matundu yote ya mwili yaani pua, njia ya haja kubwa na ndogo, mdomoni, masikioni, machoni, hali inayopelekea kifo kwa muda mfupi. Kipindi cha kuonekana kwa dalili za ugonjwa ni kati ya siku 3 hadi 9 baada ya kupata maambukizi.

Ugonjwa huu unaenea kwa urahisi sana na ha­raka kutoka mtu mmoja hadi mtu mwingine iwapo mtu atakuwa karibu na mgonjwa na kugusana na mate, damu, mkojo, machozi, kamasi, maji maji mengine ya mwili, ikiwa ni pamoja na jasho au kumgusa  mtu aliyekufa kwa ugonjwa wa Marburg.Ugonjwa huu pia unaweza kuenezwa iwapo mtu atagusa nguo au mashuka ya mgonjwa wa Marburg.

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, imechukua hatua zifuatazo katika kukabiliana na tishio la ugonjwa huu:

o   Kutoa taarifa ya tahadhari ya ugonjwa huu kupitia kwa Waganga Wakuu wote wa Mikoa na Wilaya. Aidha taarifa hii pia imejumuisha namna mgonjwa anavyoweza kutambuliwa (Ainisho la Ugonjwa),  “Fact sheet” ya ugonjwa, Mwongozo kwa watumishi wa afya wa namna ya kuchukua sampuli na vipeperushi vinavyoelezea ugonjwa huu.    

o   Kuimarisha ufuatiliaji wa ugonjwa huu kupitia kwa Wataalamu wa Afya katika Mikoa, Wilaya na maeneo ya mipaka. Aidha watalaamu hawa wa Afya pia wanatoa elimu kwa wananchi kuhusu dalili za ugonjwa huu ili endapo ugonjwa huo utatokea uweze kutolewa taarifa mapema.

o   Kupeleka vifaa kinga kwa ajili ya watumishi wa afya

Wananchi wanashauriwa kutokuwa na hofu kwani mpaka sasa hakuna mgonjwa yeyote aliyeripotiwa nchini. Wananchi wanashauriwa kutoa taarifa kwenye kituo cha huduma za afya kilicho karibu mara watakapoona mgonjwa yeyote atakayehisiwa kuwa na dalili za ugonjwa huu.

No comments:

Post a Comment