Zamani za ukoloni, palitokea Mzungu mmoja. Mzungu huyo hakuwa mtu mwema.
Alikuwa mkali na mkatili sana. Kwa ajili ya ukatili wake watu walimwita
mkoloni. Wanancgi wote walimchukia sana popote pale alipokwenda.
Mzungu huyo alikuwa Bwana Shamba. Alikuwa na bakora iliyokuwa imetengenezwa kwa
mkwaju. Kila alipokwenda kukagua mashamba, alikuwa na bakora hiyo mkononi.
Alipendelea sana kuitwa "Bwana Mkubwa". Mkolono huyo alifurahia sana
kupiga watu. Aliwapiga watu waliposhindwa kupalilia mashamba. Aliwapiga pamba
yao ilipokuwa chafu. Aliwapa taabu sana.
Katika kijiji cha Kwachaga, Wilaya ya Handeni, alikuwapo mzee mmoja aliyeitwa
Kibanga. Mzee huyu alikuwa mwenye nguvu, hodari na shujuaa. alikuwa fundi wa
mieleka. Ingawa alikuwa mwenye nguvu, alikuwa mpole. Hivyo watu wa Kwachaga
walimpenda na kumtegemea kuwaongoza vitani.
Siku moja yule Mzungu alifika Kwachaga kukagua mashamba ya mihogo. Jumbe pamoja
naye wakatembelea mashamba. Kwa bahati mbaya mwaka ule haukuwa na mvua ya
kutosha. Kwa hiyo mihogo haikustawi. Kila wakati yule Mzungu alipotazama
mashamba alitikisa kichwa na kufoka. Mwisho akamwagiza Jumbe kuitisha mkutano
wa watu wote wa kijij. Waliporudi kijijini Jumbe akapiga mbiu. Watu wote
wakakusanyika. Walipofika tu, yule Mkoloni akaanza kuwatukana, akawaambia,
"Ninyi watu weusi ni wavivu sana. Hamfanyi kazi sawa sawa. Mashamba yenu
ni mabaya sana". Jumbe akataka kumjibu ili kumweleza kwa nini mihogo
haikustawi. Kabla hajamweleza yule Mzungu alimrukia na kumpiga kofi. Kisha
akasema, "Sitaki kijibiwa na wewe, mvivu wa wavivu". Watu wote
wakakaa kimya. Hakuna aliyeweza kufanya kitu.
Kibanga akajitokeza, akasimama. Akamtazama yule Mkoloni kwa dharau sana. Kisha
akamwuliza, "Kutuita sisi wavivu ndiyo nini? Na kumpiga Jumbe wetu mbele
yetu, maana yake nini?"
Kabla ya kumaliza kusema, Mkoloni aliamka kitini kwa hasira , akataka kumpiga
Kibanga. Alishika bakora yake mkononi. Akasedma, "Nitakuadhibu vibaya kima
we! Unajifanya kuwa shujua? Huwezi kucheza na bwana mkubwa. Nitakupiga, kisha
utakwenga jela miezi sita." Lakini Mkoloni hakuwahi kumwadhibu Kibanga.
Aliadhibiwa yeye. Kabla ya kumfikia, Kibanga alimpiga chenga. Kisha akamrukia,
akamnyangánya bakorta yake. Akaitupa, ikaokotwa na vijana, wakaificha.
Kibanga alimshika yule Mzungu akamwambia. "Wewe umezoea kutoa amri kila
siku, lakini leo utashika adabu, mbwe wee!" Papo hapo alimnyanyua juu na
kumbwaga chini, puu! Yule Mkolono akaumia sana. Kabla ya kuamka, Kibanga
alimwinua tena na kumbwaga chini kama furushi la pamba. Akamkalia.
Hapo yule Mkoloni akawa hana la kufanya. Bila ya bakora alikuwa hana nguvu.
Akaomba radhi akilia, "Samahani! Naumia! Nihurumie! Sitafanya tena
hivyo." Kibanga alimjibu kwa dharau, "Sikuachi mbwa wee! Leo utakiona
cha mtema kuni! Ulijiona una nguvu. Leo nitakutengeneza."
Wazee wakamshika Kibanga na kumwomba asimpiga tena. Akamwacha. Kwa shida yule
Mkoloni akajikokota kwenda hemeni. Alikuwa amejaa vumbi huku damu zikimtoka.
Wazee wengine wakamfuata nyuma. Walinyamaza kimya, wakimhurumia. lakini vijana
walifurahi sana.
Baadaye waliimba wimbo wa kumsifu Kibanga.
Jioni yule Mkoloni aliomba radhi kwa wazee. Mzee mmoja akasimama na kumwambia,
"Umefanya vizuri kuomba radhi, nasi tunaipokea. Lakini tangu leo
usijivunie ubwana. Jivunie utu. Ninyi wakaoloni mna kiburi. Mnatudharau. Kama
ungetuuliza tungekuambia kwa nini migogo haikustawi. Haya yote yamekupata kwa
sababu ya kiburi chako. Katika nchi hii tuanaamini kuwa kiburi si
maungwana".
Baada ya hapo wazee wakamsamehe, lakini hawakumpa bakora yake. Ikabaki nyumbani
kwa Jumbe. Yule Mkoloni akaondoka. Tangu siku hiyo hakufika tena Kwachaga. Kila
mara alipokutana na watu aliyakumbuka maneno ya yule mzee, "Kiburi si
maungwana".
Siku hizi kijiji cha Kwachaga kina maendele mazuri ya kilimo na mifugo.
Maendeleo yote yamepatikana kwa sababu ya uongozi bora wa Serikali ya wananchi.
No comments:
Post a Comment