Tuesday, March 5, 2013

Mtoto wa miaka 7 aweka rekodi ya kupanda mlima kilimanjaro hadi kileleni


                                                      Mtoto Aryan Balaji (7)
 Mtoto Aryan Balaji (7), raia wa India amefanikiwa kuweka rekodi nyingine ya kufika kileleni mwa mlima Kilimanjaro, kwa kupitia barabara ya Lemosho iliyopo wilayani Siha na kushukia geti la Mweka.


Balaji anaweka rekodi nyingine ya kuwa mtoto wa kwanza mwenye umri wa miaka saba kupanda Mlima Kilimanjaro, baada ya kupanda mlima Everest uliopo nchini Nepal, ambao ni mrefu kuliko yote duniani.
Akizungumza juzi baada ya kumaliza safari yake, Balaji alisema katika safari yake amekumbana na changamoto nyingi, lakini kutokana na kuwa na waongozaji wazuri, alifanikiwa kutimiza malengo yake ya kufika kileleni.Alitaja moja ya changamoto alizokumbana nazo ni pamoja na kuwepo kwa upepo mkali, barabara kuwa na matope yanayosababishwa na mvua inayonyesha mara kwa mara, pamoja na kujishika kwenye miamba wakati wa kutembea.

“Ilikuwa kazi ngumu sana kutembea huku ukiwa unashikilia miamba wakati wa kupanda mlima, ilikuwa vigumu kuamini mtoto kama mimi naweza kumudu lakini ilikuwa rahisi kutokana na waongozaji wetu kuwa wazoefu na wenye ujuzi wa hali juu kwa kutupangia muda vizuri,” alisema.Alisema safari ya kupanda mlima Kilimanjaro ilikuwa nzuri zaidi kuliko ya Evarest, kutokana na waongozaji wa Kampuni ya utalii ya Easy Travel ya mjini Arusha, kutoa ushirikiano wa kutosha kwa kuonesha utamaduni wa Watanzania, hali iliyowafanya kufurahia zaidi kufika nchini.

Aliwashauri watoto wenzake, kutosubiri muda usogee, wakidhani ndio wataweza kufanya mambo wanayofikiria kwa sasa hivi, badala yake waoneshe nia zao mapema kwa wazazi wao ili waweze kusaidiwa kutimiza ndoto zao.Alisema kuwa baada ya kupanda milima mirefu zaidi duniani, anatarajia kuweka rekodi ya kujifunza tamaduni mbalimbali duniani, pamoja na kuzungumza na watoto wenzake kueleza alichokifanya na kufikia mafanikio yake.

Mkurugenzi wa Kampuni ya utalii ya Easy Travel ya mjini Arusha, Musaddiq Gulamhussein, alisema safari ya mtoto huyo ilianza Febuari 18, mwaka huu ambapo walitumia siku kumi kufanikisha upandaji huo wa mlima.
Musaddiq alisema mtoto huyo alifanikiwa kufika kileleni, kutokana na kumwandaa vizuri pamoja na kuwapa waongozaji wazuri kutoka kwenye kampuni yake, ambao ni wazoefu wa kuutambua mlima na njia zake vizuri.

No comments:

Post a Comment