Monday, February 11, 2013

Zitto:Spika aondolewe katika nafasi hiyo


Spika wa Bunge Anne Makinga akiongoza vikao vya Bunge mjini Dodoma

 Zitto Kabwe akihutubia mkutano wa hadhara mjini Karatu


 MBUNGE wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe amesema uamuzi wa Spika wa Bunge Anne Makinda kuifuta Kamati ya POAC ni uamuzi unaorudisha nyuma juhudi za nchi kujenga asasi za uwajibikaji.Akizungumza na Habarimpya.com Zitto alisema kwamba hatua ya Spika Makinda ni kinyume cha sheria ya ukaguzi wa umma inayotaja Kamati tatu za Bunge za kusimamia fedha za Umma na ni kinyume cha Katiba ya nchi.

"Spika wa Bunge anasema kazi za Kamati ya POAC zitafanywa na Kamati ya PAC; Tanzania ina jumla ya Mashirika ya Umma 258 yenye thamani ya shilingi trilioni 10.2 mpaka mwezi Juni mwaka 2012, hata kamati ya POAC ilikuwa haiwezi kushughulikia Mashirika yote ya Umma katika mwaka mmoja, PAC itawezaje kusimamia Wizara za Serikali, Mikoa na wakala za Serikali na wakati huo huo Mashirika ya Umma 258?"alisema Zitto na kuhoji.

Zitto Kabwe akihutubia mkutano wa hadhara mjini KaratuKatika hatua nyingine Mbunge huyo alidai kwamba, kwa vyovyote vile Taifa linarudi miaka ya kabla ya 2008 ambapo Mashirika ya Umma yalikuwa kichaka cha kuiba fedha za Umma. Hivi karibuni Kamati ya POAC iligundua mtindo wa Wizara za Serikali kupeleka fedha Serikalini kwenye Mashirika na kutumia kifisadi ili kukwepa ukaguzi kwenye Wizara (Wizara ya Utalii ilipeleka zaidi ya shilingi 600 milioni Bodi ya Utalii mwaka 2010/2011).

'Ikumbukwe pia wizi wa EPA, MEREMETA na hata uuzaji holela wa baadhi ya mali za Serikali kupitia ubinafsishaji ulifanyika nyakati ambazo Bunge halina kamati inayosimamia Mashirika ya Umma. Kwa vyovyote vile Spika wa Bunge amedhihirisha namna ambavyo anafanya maamuzi bila kuzingatia maslahi ya nchi wala kuzingatia historia ya uwajibikaji katika nchi"alifafanua Zitto.

Zitto aliongea kuwa namna mijadala ya Bunge inavyoendeshwa, namna anavyobeba ajenda za Serikali katika kujenga Bunge kibogoyo na namna anavyofanya maamuzi kwa kukurupuka, inahitaji hatua za kuokoa misingi ya uwajibikaji wa nchi. Ni lazima Spika wa Bunge adhibitiwe kwa kuondolewa katika nafasi hiyo haraka iwezekanavyo. Spika lazima ajue kwamba Mamlaka yapo kwa wananchi na yeye ni msimamizi tu wa vikao vya Baraza la wananchi liitwalo Bunge. Anna Makinda lazima adhibitiwe, vinginevyo nchi itaumia.

No comments:

Post a Comment