Mkurugenzi Mkuu wa
Mamlaka ya Uendelezaji wa Eneo Huru la Uwekezaji nchini (EPZA), Dkt. Adelhelm
Meru (aliyekaa kushoto) na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania
(TPA), Mhandisi Madeni Kipande (aliyekaa kulia) wakitia saini makubaliano ya
uendelezaji wa hekta 10 za eneo huru la bandari ya Mtwara mwishoni mwa wiki
jijini Dar es Salaam. Wanaoshuhudia ni
Waziri wa Uchukuzi, Dkt. Harrison Mwakyembe (kulia); Naibu Waziri wa Viwanda na
Biashara, Bw.Gregory Teu (kushoto) na mwanasheria wa TPA, Bi. Koku Kazaura
(katikati).
===========
========= ========
EPZA, TPA zafikia
makubaliano kuendeleza eneo huru la Bandari Mtwara
Mamlaka ya Ukanda
Maalumu wa Uwekezaji nchini (EPZA) na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA)
zimefikia makubaliano ya uendelezaji wa hekta 10 za eneo huru la bandari ya
Mtwara.Makubaliano haya ni awamu ya kwanza ya uendelezaji wa jumla ya hekta 110
za eneo hilo huru la bandari ambalo limetengwa na serikali kwa ajili ya
uwekezaji mbalimbali.
Hekta hizo 10
zitaendelezwa kwa kuwekewa miundombinu inayotakiwa na kisha kugawiwa kwa
makampuni ya kimataifa yanayofanya kazi za kutoa huduma mbalimbali kwa
makampuni yanayofanya kazi ya utafiti wa mafuta na gesi katika mkoa wa Mtwara.
Kitakapomalizika, kituo
hiki cha huduma kwa makampuni yanayofanya utafiti wa gesi na mafuta mkoani
Mtwara kitakuwa cha kipekee si kwa Tanzania pekee bali katika ukanda mzima wa
Mashariki na Kusini mwa Afrika.
Utiaji saini
makubaliano hayo ya kihistoria mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam ulifanywa
na Mkurugenzi Mkuu wa EPZA, Dkt. Adelhelm Meru na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA,
Mhandisi Madeni Kipande na kushuhudiwa na Waziri wa Uchukuzi, Dkt. Harrison
Mwakyembe na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Bw.Gregory Teu.
Akiongea wakati wa
tukio hilo, Dkt. Mwakyembe alisema hatua hiyo inatoa fursa kwa makampuni ya
kimataifa yanayotoa huduma kwa kampuni za utafiti na uzalishaji wa gesi na
mafuta kuwekeza Mtwara na pia kutoa huduma zake katika eneo hili la Afrika.
Waziri huyo alisema
tayari kampuni saba ziko tayari kuwekeza katika eneo hilo na akazitaka mamlaka
husika kuhakikisha zinafanya haraka na kwa usahihi matayarisho yote
yanayotakiwa ili kampuni hizo ziweze kuanza kufanya kazi mara moja.“Mamlaka
husika hazina budi kumaliza haraka na kwa usahihi matayarisho yanayotakiwa ili
uwekezaji huu uanze mara moja,” alisema.
Alisema kabla ya hapo
kampuni hizo zilikuwa zikitoa huduma zake kutokea Mombasa, Kenya na Afrika ya
Kusini.Waziri Teu alisema hatua hiyo ni muhimu kwa uchumi wa Tanzania.“Mtwara
na Tanzania sasa vinafunguka zaidi,” alisema, na kuongeza kuwa baada ya kuanza
kazi, kampuni hizo zitazalisha ajira kwa watanzania na kuongeza wigo wa kodi
kwa serikali.
Kwa upande wake, Dkt.
Meru alisema hatua hiyo ni muhimu sana kwa kuwa kampuni hizo zitatoa huduma kwa
makampuni yanayofanya utafiti na uzalishaji wa gesi na mafuta katika nchi za
Kusini na Mashariki ya Afrika.Alisema ujio wa kampuni hizo pia utasaidia katika
kuendeleza sekta nyingine kama hoteli na kilimo katika mkoa wa Mtwara.
Baadhi ya kampuni
zilizoonyesha nia ya dhati kuwekeza katika eneo hilo la hekta 10 ni pamoja na
Schlumberger, Weatherford and Halliburton International Inc toka Marekani;
Lena, FFF (T), Alpha group and Queensway toka Dubai na Uingereza; Altus Tanzania
Ltd toka Singapore; Tans Ocean Industries & Services Ltd toka Dubai na
Intershore Tanzania Ltd ya Afrika ya Kusini.
No comments:
Post a Comment