Zitto Kabwe
Mahakama ya rufaa kanda
ya Dar es Salaam imempa ushindi mbunge wa Kigoma kaskazini Mh. Zitto Kabwe
katika shauri lake la kupinga kamati kuu ya chama chake kujadili uanachama wake
hadi rufaa aliyokata baraza kuu la chama hicho itakaposikilizwa na kuamuliwa.
Akitoa maamuzi ya kesi
hiyo jijini Dar es Salaam jaji aliliyeendesha kesi hiyo John Utamwa amesema
amekubali madai ya Zitto Kabwe kuwa maamuzi yoyote ya kumvua uanachama yatakuwa
na madhara kwake binafsi kama mbunge wa Kigoma kaskazini na mwenyekiti wa
kamati ya bunge ya hesabu za serikali PAC.
Aidha amesema mbali na
hoja za Zitto kupata madhara lakini pia taifa litapata hasara ya kuingia kwenye
uchaguzi mdogo na kuongeza kuwa wanasheria wa Chadema walifanya makosa ya
kiufundi hasa kwenye hati ya kiapo kwa kuruhusu mwanasheria wa chama hicho
Peter Kibatala kusaini hati ya kiapo kwa niaba ya katibu mkuu wa Chadema Dk
Willbroad Slaa.
Mara baada ya uamuzi
huo wa mahakama nje ya mahakama hiyo wanasheria wa pande zote mbili wakapata
fursa ya kuzungumza na waandishi wa habari ambapo mkurugenzi wa sheria wa
Chadema, Tundu Lissu pamoja na mwasheria wa chama hicho Peter Kibatala
wameelezea kutoridhishwa na maamuzi hayo ambayo wamedai kuwa yanamfanya Zitto
Kabwe kuwa mbunge wa tatu wa mahakama baada ya Hamad Rashid wa CUF na David
Kafulila wa NCCR Mageuzi.
Kwa upande wake,
mwanasheria anayemtetea Zitto Kabwe, Albert Msando amesema amefurahishwa na
maamuzi ya mahakama kuu na kwamba wanachosubiri wao hivi sasa ni kesi ya msingi
itakayoanza kusikilizwa Februari 13 mwaka huu.
Kama ilivyo ada nje ya
mahakama hiyo kikosi cha kutuliza ghasia FFU kiliimarisha ulinzi zaidi tofauti
na jana ambapo magari ya maji ya kuwasha yalikuwa mawili, lakini hata hivyo
hayakutumika wala mabomu ya machozi kufuatia wafuasi wa pande zote mbili kutii
sheria bila shuruti baada ya kutangaziwa kutawanyika na wao kufanya hivyo.
Zitto amejikuta katika
mgogoro na chama chake cha Chadema baada ya kutuhumiwa kuwa anapanga njama za
kukidhoofisha akishirikiana na aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Arushha
Samsoni Mwigamba na aliyekuwa mjumbe wa kamati kuu Dokta Kitila Mkumbo ambao
wamevuliwa uanachama hivi karibuni.
No comments:
Post a Comment