Picha ya Maktaba ikimwonyesha Waziri wa Fedha, marehemu
Dk William Mgimwa akisoma bajeti ya wizara yake bungeni.
Ni Dk William Mgimwa, alikuwa akitibiwa
Afrika Kusini, Rais Kikwete atuma salamu za rambirambi.Dar es Salaam na Iringa.
Waziri wa Fedha na Mbunge wa Kalenga (CCM), Iringa, William Mgimwa amefariki
dunia jana katika Hospitali ya Kloof Medi-Clinic, Pretoria, Afrika Kusini
alikokuwa akitibiwa.
Habari zilizopatikana
jana kutoka Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini kupitia kwa Msemaji wake,
Habib Awesi zilisema Waziri Mgimwa amefariki dunia mchana... “Ni kweli
amefariki leo mchana tumepeleka taarifa Ikulu, Dar es Salaam.”
Baadaye jana, Katibu
Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alithibitisha kupokea taarifa za kifo hicho
na kusema Waziri Mgimwa alifariki dunia saa 5:20 kwa saa za Afrika Kusini (saa
6:20).
“Kinachofanyika kwa
sasa ni maandalizi ya kuurudisha nyumbani mwili wa marehemu na hilo linafanywa
na Serikali kwa kushirikiana na familia yake. Taarifa zaidi zitatolewa baadaye
kadiri zitakavyopatikana,” alisema Balozi Sefue.
Akizungumzia msiba huo,
Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema: “Bunge limepokea kwa masikitiko
taarifa za kifo cha Dk Mgimwa, alikuwa ni mtu mwaminifu katika kazi zake na
alishirikiana kikamilifu na wabunge katika kutekeleza kazi za Serikali. Taifa
limepoteza mtu makini aliyefanya kazi katika sekta ambayo aliisomea, jambo
ambalo lilimfanya awe na ufahamu mzuri wa mambo katika wizara (Fedha),” alisema
Ndugai.
Kikwete atuma
rambirambi
Jana jioni Rais Jakaya
Kikwete alitoa taarifa akielezea kushtushwa na kifo cha Waziri Mgimwa.
“Nimepokea kwa mshtuko
na huzuni kubwa taarifa za kifo cha Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa,”
ilisema taarifa yake kupitia Kurugenzi ya Mawasiliano, Ikulu.
Alisema taifa
limempoteza Waziri Mgimwa katika kipindi lilipokuwa linamhitaji zaidi kutokana
na mchango wake mkubwa ambao amekuwa akiutoa kupitia nafasi zake za Waziri wa
Serikali na mwakilishi wa wananchi wa Jimbo la Kalenga.
Katika salamu zake
kupitia kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na kwa familia ya marehemu Mgimwa, Rais
Kikwete alisema: “Sina maneno ya kutosha kuelezea mshtuko na huzuni yangu kubwa
kufuatia taarifa za kifo cha Mgimwa.
“Binafsi nilimtembelea
mara mbili hospitali alikokuwa amelazwa na mara ya mwisho hali yake ilikuwa
imeimarika. Tulizungumza kwa kiasi cha dakika 10 hivi akanielezea nia yake na
tamaa yake ya kurejea nyumbani kwa sababu hali yake ilikuwa nzuri.
“Sote tunajua mchango
wake katika Serikali. Sote tulitamani kuendelea kuwa naye, lakini haya ni
mapenzi ya Mungu... Natoa pole nyingi na rambirambi zangu za dhati kwa wana
familia wote kwa kuondokewa na mhimili wao. Naungana nanyi katika kuomboleza
msiba huo mkubwa. Napenda mjue kuwa msiba huu ni msiba wangu pia. Machungu yenu
ni majonzi yangu,” alisema Rais Kikwete.
No comments:
Post a Comment