Umoja wa Mataifa umeelezea wasi wasi dhidi ya usalama wa mji wa kale wa Timbuktu kaskazini mwa Mali huku machafuko yakiendelea eneo hilo.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi na Utamaduni{UNESCO} limesema Timbuktu na kaburi la Askia ambalo limekuwepo tangu karne ya 17 katika mji wa Gao ni maeneo yanayokumbwa na hatari. Makundi ya Kiisilamu yameuteka mji wa Gao kutoka kwa waasi wa Tuareg.
UNESCO imeelezea hofu ya tisho la kuporwa kwa baadhi ya kumbukumbu za kale ambazo zimehifadhiwa maeneo hayo.Serikali ya Mali imetaka Umoja wa Mataifa kutambua tisho la usalama wa maeneo ya kale na kusema huenda kukawa na biashara ya magendo ya vifaa vya kale.
Mji wa Timbuktu ambao uko kwenye Jangwa la Sahara una maeneo mengi ya kale ambayo yamedumu kwa karne nyingi licha ya kujengwa kwa udongo na mbao. Mji huo pia umehifadhi nyaraka za kale laki saba kwenye maktaba 60.
Waasi wa Tuareg na wapiganaji wa Kiisilamu wameweza kuyadhibiti maeneo ya Kaskazini mwa Mali baada ya kutokea mapinduzi wa kijeshi nchini humo.
Wadadisi wamesema makundi hayo yana misimamo tofauti ambapo Tuareg wanakata kujitenga huku kundi la Kiislamu likitaka kuwepo Sharia ya Kiisilamu kote nchini Mali.
Kaburi la Askia, lilijengwa mwaka 1495 kwa umbo la Piramidi ambapo amezikwa Mfalme Mohammad Askia, aliyeongoza Milki ya Songhai, ambayo imetajwa kua bora zaidi katika historia ya Milki za Kiisilamu.
No comments:
Post a Comment