Baadhi ya wahamiaji
haramu waliolazimishwa kurejea makwao na Tanzania
Umoja wa Mataifa umesema kuwa takriban wahamiaji
haramu elfu 25 kutoka Burundi wameondoshwa Tanzania kwa nguvu katika mwezi
mmoja uliopita.
Afisa wa shirika la Umoja wa Mataifa la
kuwahudumia wakimbizi UNHCR amesema malori yanayowasafirisha warundi yamekuwa
yakivuka mpaka kila siku , huku wahamiaji haramu wengi wakikosa mahitaji muhimu
kama vile maji na chakula
Katika wiki za hivi karibuni, Tanzania imekuwa
ikiwarejesha makwao kwa nguvu wale walioelezwa wahamiaji haramu kutoka Burundi,
Rwanda na Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Kwa miaka mingi Tanzania iliwahifadhi
mamilioni ya wakimbizi waliokuwa wakiyakimbia mapigano katika nchi jirani .
Takriban watu milioni moja walitoroka kutoka
Burundi na kuingia Tanzania wakati wa mgogoro wa wenyewe kwa wenyewe wakati
vita vilipozuka mwaka 1993. Wengi walirejea kwa hiari wakati amani
ilipopatikana mwaka 2006.
Nchi hiyo imekuwa makao kwa mamilioni ya
wakimbizi katika kipindi
cha zaidi ya miaka kumi iliyopita kutokana na migogoro
katika eneo la maziwa makuu.
Maafisa wa Tanzania sasa wameanza kutekeleza
amri ya kuwaondoa kwa nguvu wale wanaodaiwa kuwa wahamiaji haramu kutoka
Burundi, Rwanda, na Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo.
Shughuli hii imetokea wakati mmoja na mgogoro
wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Rwanda ambayo imekuwa ikikanusha madai ya
kuchochea vurugu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Mgogoro ndani ya Jamhuri ya kidemokrasia ya
Congo nao unaendelea kuchochea idadi ya wakimbizi wanaotoroka vita na kuingia
katika nchi jirani.
No comments:
Post a Comment