DAR ES SALAAM.
Maandalizi
ya ujio wa Rais wa Marekani, Barack Obama nchini yanazidi kupamba moto huku
maofisa wa usalama wa Marekani wakipiga kambi katika Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.
Aidha, kutokana na ujio huo, Serikali imeagiza
mashirika yote ya ndege kubadili ratiba zao za safari Julai Mosi, siku ambayo
Rais huo atatua nchini.Jana, waandishi wetu walishuhudia pilikapilika za
kuimarisha ulinzi katika uwanja huo jambo ambalo uongozi wa uwanja huo jambo
wamelieleza kwamba halijawahi kutokea.
Ulinzi
haijawahi kutokea
Mkurugenzi
wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Moses Malaki alisema jana
kwamba ratiba za uwanjani hapo zitabadilika kutokana na uzito wa ugeni huo.Alisema
kwa kawaida anapokuja kiongozi mkubwa wa kitaifa katika uwanja huo hakuna ndege
inayoruhusiwa kutua kwa kipindi cha nusu saa.
“Ni kweli hali hiyo pia itakuwapo atakapokuja
Rais Obama na safari za ndege zitabadilika kulingana na ratiba ya kutua na
kuondoka kwa Rais huyo,” alisema Malaki.Pia alisema ulinzi katika uwanja huo
umeimarishwa kwa mwezi mmoja sasa na tangu wakati huo, maofisa wa usalama wa
Marekani wamekuwa wakifika kwa nyakati mbalimbali.
“Sijawahi kuona ulinzi mkali kama huu,
wamekuja marais wengi hapa nchini lakini ulinzi huu ni wa kutisha, sijui kwa
sababu gani?” alisema Malaki.
Alisema awali, wakati maofisa hao walipoanza
kuwasili nchini hawakutambua ni mgeni gani anayetarajia kufika lakini baadaye
walipelekewa taarifa kuwa ni Rais Obama na baadaye walitaarifiwa kuwa angetua
saa 8.40 mchana, Julai Mosi.
Mkurugenzi
huyo alisema Rais Obama atakuja na ndege nne, moja itakayombeba, ya pili kwa
ajili ya mizigo, ya tatu itakuwa ya waandishi wa habari na maofisa wa usalama
na ya mwisho ni kwa ajili ya dharura ambayo itaegeshwa katika Uwanja wa Ndege
wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Malaki
alisema maofisa wa Marekani wanaowasili nchini wamekuwa wakifanya shughuli
mbalimbali za kuhakikisha kuwa hali ya usalama inaimarishwa na kuwaacha wazawa
wakifanya shughuli za kawaida.
“Ulinzi ni mkali mno, yapo masharti kadhaa
wanayoyataja kuwa yatatumika kwa watu watakaoingia eneo la uwanja au kuisogelea
ndege ya Rais Obama. Jamaa wameweka masharti magumu,” alisema.
Mkurugenzi
huyo alisema maofisa hao wanakuja kwa makundi na hivi karibuni lilifika kundi
la kusimamia mawasiliano ambayo yatatumiwa wakati watakapokuwa nchini.
“Pia
wamechukua kwa muda karakana ya Shirika la Ndege la Precision Air iliyoko
kwenye eneo la Uwanja wa Ndege. Maofisa wa Usalama wa Marekani wanataka kufanya
shughuli ndani mle,” alisema Malaki.
Pia,
ndege mbovu zilizokuwa kwenye maeneo ya uwanja huo zimeondolewa. Viongozi wa
Precision Air hawakupatikana kuzungumzia suala hilo.
Mkurugenzi
wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Fadhili Manongi alisema ni utaratibu
wa kawaida kwa karakana kuazimwa wakati wanapokuja wageni mashuhuri.
“Nafasi
ile mara nyingi hutumiwa na maofisa wa usalama pale wanapokuja wageni mashuhuri
kwenye Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere,” alisema.
Alidokeza
pia pamoja na ugeni wa Rais Obama, pia kumekuwa kuna presha ya ugeni wa marais
wa nchi mbalimbali duniani wanaokuja kuhudhuria mkutano wa Smart Partnership
unaonza keshokutwa.
Pia
wana kazi ya kuwapokea wake za marais wa Afrika watakaokutana na mke wa Rais
Obama, Michelle na mke wa Rais wa zamani wa nchi hiyo, George Bush, Laura.
Kazi
inayofanyika
Ofisa
mmoja wa Uwanja Ndege ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema maofisa hao
walifanya ukaguzi wa hali ya juu kwenye sehemu mbalimbali za uwanja huo
wakitumia mitambo maalumu ya kung’amua mabomu.
“Hawa
jamaa wako juu sana katika mambo ya usalama maana wana kifaa cha kuchunguza
mabomu hata yaliyo chini ya ardhi,” alisema na kuongeza kuwa licha ya kukagua
uwanja huo, pia walikwenda mbali zaidi na kukagua maeneo ya jirani.
Mitambo
mbalimbali ya shughuli za usalama imefungwa kwenye eneo hilo la uwanja na
maofisa wa Marekani walionekana wakiwa juu ya paa la moja ya majengo ya uwanja
huo wakifunga mitambo katika minara mirefu kwa ajili ya kuimarisha mawasiliano.
Yavuruga
ratiba za ndege
Manongi
alisema kampuni za ndege zimeagizwa kufanya mabadiliko ya ratiba za safari siku
atakapowasili Rais Obama ili kutoa nafasi kwa anga hilo kutumika kwa shughuli
za mapokezi yake.
Alisema
kampuni zote za ndege zimeshapewa taarifa kuhusu hatua hiyo.
“Kubadilishwa
kwa ratiba kunatokea mara kwa mara na huwa tunawapa taarifa kampuni za ndege
mapema ili wajue namna ya kujipanga,” alisema Manongi.
Kutua
Senegal leo
Rais
Obama anatarajiwa kuanza ziara yake ya barani Afrika leo na alitarajiwa kutua
Dakar, Senegal saa 9.30 alasiri kwa saa za Afrika Mashariki.
Akiwa
nchini humo, ratiba inaonyesha kuwa atakuwa na mazungumzo na Rais wa Senegal,
Macky Sall kwenye Ikulu ya nchi hiyo. Pia ratiba hiyo inaonyesha kuwa atakutana
na majaji kutoka mikoa yote ya nchi hiyo.
Pia
atakwenda katika Kisiwa cha Goree ambacho kiko kwenye Bahari ya Atlantic na
atatembelea Jumba la Makumbusho katika kisiwa hicho ambacho kilikuwa kituo cha
kuhifadhi watumwa waliokuwa wanasafirishwa kutoka Afrika kwenda Marekani.
“Baada
ya shughuli hiyo, Rais Obama atahudhuria dhifa ya taifa kabla ya kupumzika kwa
muda mfupi na kuanza safari ya kwenda Afrika Kusini,” ilisema taarifa hiyo ya
Ikulu ya Marekani.
Chanzo:
mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment