Friday, June 7, 2013

UGANDA: UKIMWI KUPIMWA NYUMBA HADI NYUMBA





KAMPALA.

Kampeni ya kupima virusi vya ugonjwa wa Ukimwi, imeanza kwenye makazi ya watu na maeneo yenye mkusanyiko mkubwa wa biashara nchini Uganda.


Kampeni hiyo ya kupimwa virusi hivyo ilianza jana kwa watalaamu kupita nyumba kwa nyumba na maeneo yenye mkusanyiko wa biashara. Mratibu wa kampeni hiyo, Possy Kyiira kutoka Wizara ya Afya alisema watafanikiwa iwapo watu watajitokeza kupima virusi hivyo bila uwoga.Alisema waratibu wake watakuwa na gari maalumu ambalo pia litakuwa likizungukia watu walioko makazini na sehemu zao za kazi.

Alizitaja sehemu hizo kuwa ni pamoja na sehemu zenye mkusanyiko kama kwa waendesha bodaboda, madereva taksi, mafundi gereji wanawake wanaojiuza pamoja na wale wanaume waliokuwa na tabia za kutembea na wanaume wenzao. Alisema maambukizo ya ugonjwa huo nchini humo yanaongezeka siku hadi siku hivyo kinachotakiwa ni kuhakikisha wanadhibiti hali hiyo. Prossy Kayiira, aliongeza kwamba watakachokuwa wakikifanya ni kutoa ushauri nasaha 

kwa watu walioathirika na wasioathirika ili kuepuka ugonjwa huo usiendelee kuua wananchi wa Uganda.  “Watu wengi wanajisikia aibu kupima Ukimwi hata kutembelea vituo vya afya kwa ajili ya kupimwa, sasa sisi tunajitolea kuhakikisha tunawafikia mpaka nyumbani na sehemu zao za kazi,” alisema.

Mwaka  2011 utafiti ulionyesha kwamba kiwango cha waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi nchini humo kilipanda mpaka kufikia asilimia 7.3, ambapo ilipanda kutoka asilimia 6.4 tangu mwaka 2006.

Chanzo: mwananchi.co.tz

No comments:

Post a Comment