Wednesday, June 5, 2013

KIBANDA: MSINILILIE


.Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania, Absalom Kibanda (aliyevaa miwani katikati), akizungumza na waandishi wa habari Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jana mara baada ya kurejea kutoka Afrika Kusini

HATIMAYE Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na Mhariri Mtendaji wa New Habari (2006) Ltd, Absalom Kibanda, amerejea nchini na kuvitupia lawama vyombo vya usalama kwa kushindwa kuwakamata watu waliomtesa na ambao wamekuwa wakitekeleza mauaji ya wanahabari nchini. Kibanda alitoa kauli hiyo jana, katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA), baada ya kuwasili akitokea nchini Afrika Kusini, alikokuwa akitibiwa baada ya kushambuliwa na kujeruhiwa vibaya na watu wasiojulikana, Machi 6, mwaka huu.
Alisema anashangaa Jeshi la Polisi kushindwa kuwakamata wahalifu hao kwa zaidi ya siku 90 alizokuwa amelazwa akitibiwa, licha ya kuahidiwa na Mkuu wa Jeshi hilo (IGP) Saidi Mwema, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, kuwa watalishughulikia suala hilo haraka.
“Waziri alinitembelea Afrika Kusini akaniahidi atalifanyia kazi suala hili, Kamanda Kova na IGP Mwema pia waliniahidi hivyo wakati nikiwa nimelazwa Muhimbili, lakini hadi leo ni siku 90 zimepita bila majibu yoyote.“Litakuwa ni taifa gani kama mtu anaweza kumng’oa mtu jicho, meno, kucha, kumkata kidole, kumvunja taya na mifupa nane na kuachwa hivi hivi pasipo kunyooshewa kidole.
“Hadi sasa bado namuuliza Mungu, ni kwa nini aliruhusu niwe hai hadi leo, labda niokoe taifa langu,… Waandishi wa habari wenzangu, msinililie mimi, lililieni taifa lenu ambalo ndani ya miaka nane ya utawala huu matukio mengi yametokea lakini hakuna linalofanyika,” alisema.
Alisema ufafanuzi kuhusu tukio lake hilo, atazungumzia siku nyingine Mwenyezi Mungu akimpa uzima. Kibanda alisema tangu tukio hilo lilipotokea, mengi yamesemwa, huku wengine wakilihusisha na vyama vya siasa, kazi yake pamoja na usalama wa taifa.
“Bado nina maumivu ya mwili, lakini sina maumivu ya moyo, vita hii si ya miili na nyama, tuna wajibu wa kuokoa taifa letu, na kuhusu tukio langu hili nitalisemea mimi mwenyewe pasipo kumnyooshea mtu kidole…Waingereza wanasema ‘everything for a purpose’, namwachia Mungu,” alisema.
Pia alisema, tukio la kuteswa na kujeruhiwa kwake pamoja na waandishi wa habari wengine siyo matukio ya bahati mbaya, kwani mengi yanafanana.
“Saed Kubenea alipovamiwa, Daudi Mwangosi alipouawa, Shabaan Matutu alipovamiwa na kupigwa risasi na polisi, Mnaku Mbani aliposhambuliwa na matukio mengine ya namna hii kwa wanahabari, nataka niwahakikishie waandishi wa habari wenzangu kuwa matukio haya si bahati mbaya.
“Pia, tukio hili linafanana sana kimazingira na tukio la kutekwa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka.“Wanahabari wenzangu, machozi ninayoyatoa hapa leo si kwa sababu tu ya maumivu niliyoyapata, bali ni kutokana na mshikamano ninaouona hapa leo,” alisema Kibanda.

Aliwaasa wanahabari nchini kuendeleza mshikamano waliouonyesha katika tukio lake tangu alipojeruhiwa hadi walipompokea jana kwa nia ya kulifanya kuwa tukio la mwisho la majonzi kwa wanahabari.
Alisema katika vita ya kupinga vitendo vya utesaji na uuaji watu wasiokuwa na makosa, wanahabari wanapaswa kutokata tamaa wala kushindwa, kwa sababu taifa linapitia katika kipindi kizito, hivyo ni jukumu la wanahabri kuliokoa.
Aidha, Kibanda alivishukuru vyombo vyote vya habari nchini na Watanzania kwa ujumla kwa kumuombea katika kipindi kigumu cha maumivu makali alichopitia hadi kurejea nchini.
“Sitaki kuwa mbinafsi nisipowashukuru ninyi na Watanzania wenzangu, wengi ni mashahidi wa hali niliyokuwa nayo, kuna matukio mengine nimeyaona kwenye picha, sikuwa na fahamu sawa sawa.
“Napenda kuwashukuru wanaonifahamu na wasionifahamu kwa kunitia moyo na kunifariji, shukrani za dhati kwa Kampuni yangu ya New Habari (2006) Ltd, na Ofisa Mtendaji Mkuu wake Hussein Bashe, kwa namna alivyohakikisha anafanikisha matibabu yangu nikiwa Afrika Kusini.
“Napenda kuwashukuru Jukwaa la Wahariri kwa kazi ngumu waliyoifanya ya kuunda Tume na hata kunitembelea nchini Afrika Kusini, ni vigumu kumtaja mmoja mmoja lakini zaidi nawashukuru Watanzania wote kwa namna ya pekee,” alisema.Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, Hussein Bashe, alisema usalama wa Kibanda ni usalama wa Kampuni, hivyo ni jukumu lake kuulinda.
Kibanda alirejea jana majira ya saa nane mchana na kulakiwa na umati wa waandishi wa habari waliofurika uwanjani hapo sambamba na Watanzania wengine walioguswa na tukio alilotendewa.Kibanda alibubujikwa na machozi baada ya kukutana na umati wa wanahabari waliofika kumlaki, hali aliyoelezea kuwa ni kutokana na ushirikiano ambao waandishi hao wameuonyesha kwake.
Kibanda alivamiwa na kuteswa Machi 6 mwaka huu na watu wasiofahamika, wakati akirejea nyumbani kwake Goba Punguni, Kata ya Mbezi Juu, jijini Dar es Salaam, ambapo alijeruhiwa vibaya kwa nondo, mapanga na kisha kung’olewa meno, kucha na kumharibu jicho la kushoto na taya.

No comments:

Post a Comment