Vicky Kimaro, Mwananchi
Dar es Salaam.
“Madaktari waliponiambia kuwa watoto wangu wameungana nilichanganyikiwa,
niliona dunia imenigeuka, sikuwahi kuwaza nitakutana na kitu cha namna hii
katika maisha yangu.”
Ni maneno ya binti
kutoka kabila la Wandali ambalo asili yake ni Mbeya, Grace Joel (19), ambaye
Februari 20 mwaka huu, alijifungua mapacha wa kiume ambao wameungana katika
sehemu ya kiunoni.
Mwanadada huyo anasema
hakuamini macho yake pale madaktari wa Hospitali ya Uyole iliyopo mkoani humo
walipomwambia kuwa watoto wake wameungana na hivyo kupewa rufaa ya kwenda
kwenye Hospitali Kuu ya Mkoa wa Mbeya.
"Wakati wa
ujauzito wangu sikuwahi hata siku moja kuhisi kuwa ningeweza kuzaa watoto
wakiwa kwenye tatizo hili, sikuwahi kuumwa zaidi ya kuvimba miguu tu na hiyo ni hali ya kawaida kwa mjamzito
yeyote." anasema Grace ambaye kwa sasa anahitaji msaada wa hali na mali
ili kuokoa maisha ya watoto wake.
Licha ya umri huo
mdogo, amejikuta kwenye hali ya mateso na uchungu mwingi baada ya familia yake,
hususani mume wake, Erick Mwakyusa kumtelekeza kwa kile alichodai kuwa hana
haja na watoto walioungana.
"Nilishangaa,
familia yangu kunitelekeza katika hali hii baada ya kugundua watoto wameungana,
mume na familia yake alinitamkia wazi kuwa hawana shida na watoto walioungana,
alisema hawezi kuwalea kwa kuwa kwao hakuna watoto wenye ulemavu wa aina hiyo,”
anasema.
"Siyo siri
nilisijikia uchungu, sikuamini kuwa mume wangu angenifanyia hivyo, siyo yeye tu
hata familia yao yote sikudhani kama wangenigeuka hivyo, nashukuru kwa upande
wa familia ya wazazi wangu walikuwa pamoja nami ingawa ni maskini na hawana
uwezo wa kunisaidia.
"Hospitali ya
Kyela ndiyo iliyonipeleka ile ya Rufaa Mbeya ambao nao walivyoona hali ya
watoto wangu wakanishauri kuja Muhimbili, sikuwa na uwezo wa kufika hapa,
lakini nawashukuru madaktari wa Rufaa Mbeya walioniwezesha kufika hapa.
Grace anasema watoto
wake hao, Elikana na Eliud aliwazaa wakiwa na uzito kilo tano na nusu na
walifika Hospitali ya Taifa Muhimbili wiki mbili tangu kuzaliwa kwao.
Wanatumia njia moja
kujisaidia
Dk Zaituni Bokhari,
ambaye ni Daktari Bingwa katika Kitengo cha Upasuaji kilichopo Hospitali ya
Taifa Muhimbili, anasema kutokana na namna walivyoungana, wanatumia njia moja
kujisaidia.
"Njia ya kukojolea
wanatumia moja na pia njia ya haja kubwa wanatumia moja, tutakapowatenganisha
kuna utaalam ambao utafanywa ili kila mtu aweze kutumia njia yake mwenyewe bila
athari zozote," anasema.
Anaeleza kwamba, iwapo
upasuaji huo utafanikiwa watoto hao watakuwa kule India kwa wiki mbili ndipo
watarejea nchini na kuendelea na
matibabu chini ya uangalizi wa wataalamu wa Hospitali ya Muhimbili hadi pale
afya zao zitakapoimarika.
Kutokana na hali ya
kiuchumi ya mama huyo, Dk. Bokhari
amewataka wasamaria wema kujitokeza na kutoa misaada mbalimbali kama ya maziwa,
nguo na fedha kwa ajili ya vitu vidogo vidogo ili aweze kuwahudumia vyema
watoto wake.
Dk. Bokhari anasema wao
waliwapokea watoto hao wakiwa katika hali mbaya kutokana na uchovu wa safari
kwa basi kutoka Mbeya na walikuwa na maambuzi sehemu mbalimbali.
“Walikuwa ni wachanga
kabisa, walikuwa na wiki mbili, walikuwa wamechoka kutokana na mwendo mrefu wa
basi kutoka Mbeya, walikuwa na homa kali na matatizo katika njia ya kupumua,
tukatibu kwanza matatizo hayo ndiyo vipimo vingine vikaendelea,” anasema.
"Wamefika hapa
hawakuwa hata na nguo za kutosha, huyu mama naye alikuja katika hali ya
kuchanganyikiwa ukizingatia ukweli kuwa ndugu zake wamemtelekeza, tumefanya
kazi kubwa sana ya kumpa ushauri nasaha mpaka akakubalina na hali halisi.
"Kuna wakati
alikuwa anasema anataka kuondoka awaache watoto kwetu, hali hiyo ilitokana na
kuchanganyikiwa, muda mwingi alikuwa akilia ila kwa sasa namshukuru Mungu yeye
na watoto wanaendelea vizuri,” anasema.
Kwa nini wameungana
Dk Bokhari anasema hali ya watoto kuungana siyo ya kurithi kama
yalivyo kwa baadhi ya magonjwa.
"Hali hii inaweza
kusababishwa na upungufu wa madini,” anaeleza.
Mtaalamu mwingine wa
afya ameiambia Mwananchi kuwa, “Mapacha wanaofanana kwa kawaida hutokana na yai
lililopandikizwa kujigawa mara mbili, baada ya siku 12 mgawanyiko wa seli
(chembe chembe) unakuwa umeanza kujipanga kwa ajili ya kujiachanisha katika
uumbwaji wa viungo au ogani mbali mbali za mwili”.
Anasema kuwa, jinsi
siku zinavyozidi kusogea mgawanyiko wa mapacha kujiachanisha na kujitegemea
ikitokea kabla ya seli kufikia wakati wa kuruhusu jambo hilo, ngozi nyembamba
za mapacha hao huendelea kuungana na kushikamana.
“Hata hivyo kwa sayansi
ya tiba chanzo kikuu hasa hakijulikani,” anaeleza mtaalam huyo.
Matibabu ni India
pekee?
Dk Bokhari anasema
kutokana na aina ya upasuaji wa watoto hao, inabidi ufanyike kwenye nchi zenye
watalaamu na vifaa vya kisasa kama India au Afrika Kusini.
"Upasuaji huu
unatakiwa ufanywe na madaktari zaidi ya saba na kila daktari atakabiliana na
kiungo chake, mimi pia ni miongoni mwa madaktari ambao nitashiriki
upasuaji wa watoto hawa na inatakiwa
umakini wa hali ya juu,” anasema.
Anaeleza kuwa, upasuaji
wa aina hiyo unaweza kufanyika kwa saa 24 ama chini ya hapo.
No comments:
Post a Comment