Thursday, June 13, 2013

KAULI YA SERIKALI KUHUSU TIMU ZA SOKA KWENDA DARFUR, SUDAN


AMOS MAKALA




 DODOMA

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imezikataza timu zake kushiriki katika michuano ya CECAFA katika kuwania kombe la Kagame 2013 ambayo imepangwa kufanyika huko Darfur nchini Sudan, kutokana na sababu za kiusalama.

Kauli hiyo imetolwa leo, Jumatano, Juni 13, 2013 Bungeni na Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mhe. Amos Makala (Mb), alipokuwa akijibu swali la Mhe. Richard Ndasa aliyetaka kujua msimamo wa Serikali kuhusu ushiriki wa timu za Tanzania kwenye michuano hiyo.

Wiki jana pia Rais wa TFF, Leodegar Tenga ambaye pia ni Mwenyekiti Shirikisho la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati, CECAFA ambao ndiyo waandaaji wa michuano hiyo, alipozungumza na wanahabari kuhusu suala hilo alisema walikuwa wanasubiri kauli ya Serikali: “...tunachosubiri sasa hivi, ni position ya Serikali. Hawa ni Watanzania. Kuna vyombo vingine ambavyo ndivyo vyenye mamlaka ya kusimamia usalama wao, hili siyo suala la TFF... viongozi wetu wakituambia salama u salmini, tutawapeleka vijana wetu...”

Makala akasema:
Ni kweli, kwamba kumekuwa na taarifa za kutokuwa na hali ya usalama huko Darfur, Sudan.
Na, nimshukuru sana Waziri wa Mambo ya Nje alilitolea kauli suala hili, na sisi ndani ya Serikali tunazo taarifa za kutosha, kwamba Sudan hakuna usalama, na nchi nyingine zimeendelea kujitoa, na msimamo wa Serikali, hatuwezi kupeleka timu mahali ambapo hapana usalama.

Kwa uamuzi huo, Yanga wamevuliwa rasmi ubingwa wa michuano hiyo waliokuwa wakiushikilia kwa miaka miwili mfululizo.

No comments:

Post a Comment