Friday, July 12, 2013

MIMBA ZA UDOGONI BALAA KWA MAENDELEO, 277 WAKOSA MASOMO KWA MIMBA UNGUJA


Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi- Zanzibar



Mimba za udogoni zimeelezwa kuwa ni kikwazo kikubwa cha ukuaji wa uchumi kwa nchi masikini ikiwemo Tanzania .

Akitoa taarifa ya siku ya Idadi ya Watu Duniani leo mjini Zanzibar , kwa niaba ya waziri wa Fedha wa SMZ Omari Yusufu Mzee, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Zanzibar Dr. Mwinyihaji Makame Mwadini, amesema mimba hizo zimekuwa zikiathiri mipango ya kimaendeleo kwa nchi masikini.

Amesema Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi za bara la Afrika zenye idadi kubwa ya wasichana wanaopata mimba za utotoni wakiwa shuleni na wale wasiosoma, imebaini kuwa mamba hizo ni kikwazo katika mipango ya maendeleo ya uchumi mikoani. 
Amesema kwa mfano Zanzibar , wanafunzi wa shule za msingi na Sekondari wenye umri kati ya miaka 12 na 18 wamekuwa wakiacha masomo kutokana na kupata mimba wakiwa shuleni.

Amesema nyingi ya mimba hizo zimekuwa zikipatikana pasipo matarajio na mipango kwa watoto hao ambao wameingia katika kundi la wazazi ambapo amesema ni matokeo ya kuanza ngono utotoni zisizo salama.

Dr. Mwinyihadi amesema mimba za utotoni humkosesha mtoto wa kike elimu ya lazima na kumdumaza kimaisha wa kuanza mapambano mapema ya kujitegemea binafsi kimaisha na kuzorota kwa ukuaji wa kiuchumi kwa taifa.
Amesema pamoja na taarifa za wasichana 8,000 kuacha shule kila mwaka hapa nchini kwa mimba, lakini idadi hiyo ni ndogo ikilinganishwa na wasichana wanaoozeshwa na wazazi wao kwa watu waliowafanyia ukatili wa kingono.

Amesema katika kipindi cha miaka mitano kuanzia 2008 hadi 2012, wasichana 659 waliacha masomo katika mikoa mitano ya Unguja na Pemba ambapo kati ya hao, watoto 277 waliacha masomo kutokana na ujauzito na wengine 382 waliolewa wakiwa shuleni.

Hata hivyo Dr. Mwinyihadi amesema ili kukomesha vitendo vya unyanyasaji kwa mtoto wa kike, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeanzisha vituo vijulikanavyo kama Mkono kwa Mkono katika mikoa ya Unguja na Pemba ambapo yeyote anayefanyiwa ukatili wa kijinsia hutoa ripoti na hatua kuchukuliwa kwa mkosaji.

Amesema hatua hiyo imewafumbua macho wananchi na hata kupunguza kwa kiasi kikubwa vitendo vya unyanyasaji kwa mtoto wa kike visiwani humo.
Kauli mbiu ya mwaka huu iliyotolewa na Shirika la Kimataifa la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA) ni kila mmoja wetu lazima kushiriki kukomesha mimba za utotoni (Adolescent Pregnancy).

NAMBA ZA SIMU ZA MWANDISHI WA HABARI HII NI HIZI> 0715 886488, 0784 886488, 0767 886488

No comments:

Post a Comment