moja ya hoja ambazo huleta mabishano makubwa kwenye vijiwe vya mchezo wa soka ni ubora wa ligi barani ulaya , huu ni ubishi ambao haujawahi kupata ufumbuzi na umekuwa ukiendelea miaka nenda rudi na hakuna dalili yoyote ya kuisha kwa ubishi huu .
inawezekana ikawa vigumu kutambua
ubora halisi wa ligi hasa kwenye kiwango , matokeo na mafanikio lakini
linapokuja suala la biashara na kutengeneza mapato kutokana na mchezo wa mpira
wa miguu hakuna shaka yoyote kuwa ligi kuu ya england inaongoza na wengine
wanafuatia .
msimu uliopita bingwa wa ligi ya
england ambaye alikuwa manchester united alitengeneza jumla ya paundi milioni
60 kutokana na mapato yatokananyo na mkataba mnono wa televisheni , kama hiyo
haitoshi timu iliyoshika mkia ambayo ilikuwa queens park rangers pamoja na
kushuka daraja iliondoka kwenye ligi kuu na kifuta jasho cha paundi milioni 30
chanzo kikiwa kile kile fedha za haki za matangazo ya moja kwa moja kwenye
televisheni .
kama unadhani fedha hizo zilikuwa
nyingi basi fungua masikio vizuri na usikilize kinachofuatia …. kampuni ya ligi
kuu ya england imesaini mkataba mpya wa haki za matangazo ya televisheni ambao
thamani yake ni paundi bilioni 5.5 , hizi ni fedha nyingi sana na wale usitake
tuanze kusumbuana na vikokotozi tukijaribu kung’amua kiasi cha fedha hizi kwa
kufananisha na fedha yetu ya madafu .
matokeo ya mkataba huu mpya ni kwamba
bingwa wa ligi ya england kwa msimu tunaoungojea utakaoanza agosti 13 atavuna
karibu paundi milioni mia moja huku yule atakayeshika mkia akilamba karibu paundi
milioni 60 , fedha , fedha ,fedha zaidi .
kama umefuatilia kwa karibu
purukushani za usajili zinazoendelea hivi sasa utagundua kuwa ligi ya england
imekuwa kivutio kikubwa. pamoja na na nyota kama thiago alcantarra na gonzalo
higuain kuzitolea nje manchester united na arsenal bado ligi hii imeweza
kuwavuta wafungaji wawili bora wa ligi ya uholanzi wilfred bony na jozy
altidore , tumeshuhudia mchezaji mwenye uzoefu wa timu ya taifa ya italia
emanuele giacherini naye akitafuta makazi huko kaskazini mashariki na kipa
aliyeiongoza uholanzi
kucheza fainali ya mwisho ya kombe la dunia marten
stekelenburg naye akihamia london , hawa ni wachache kwenye orodha ndefu ambayo
pia imewashuhudia wachezaji wawili bora wa sevilla pamoja na fiorentina
wakivutwa kwenye visiwa vya malkia .
timu kama west ham united imekuwa na
msuli wa kupata jeuri ya kujaribu kumnunua striker mwenye ubora wa kiwango cha
juu kama pablo daniel osvaldo huku pia wakijaribu kumvuta alvaro negredo wote
hawa bila mafanikio , jiulize wamepata wapi uthubutu huu , jibu ni moja mambo
ya fedha .
mikataba ya televisheni imenufaisha
sana timu za ligi kuu ya england kuanzia zile za juu mpaka za daraja la kati na
zile za madaraja ya chini . na ndio maana msimu huu kumekuwa na rekodi za
vilabu saba tofauti za usajili zimevunjwaq na hakuna timu ambayo imelazimika
kwenda kusajili mchezaji toka ligi daraja la kwanza ukaichilia mbali manchester
united waliomchukua wilfred zaha katikati ya msimu uliopita .
fedha inaongea na inaongea kwa sauti
ya juu hali ya kuvifanya vilabu vya england kuwa na jeuri kubwa ya fedha na
jeuri hii inaongezeka siku hadi siku .
No comments:
Post a Comment