Katibu Mkuu Dk.
Willibroad Slaa ameendelea na ziara yake kwa kutembelea vijiji vya majimbo
mawili Bukene na Nzega, wilayani Nzega, Mkoa wa Tabora, ambapo ametumia mkutano
mkubwa wa hadhara mjini Nzega kutoa maagizo kwa viongozi wa chama nchi nzima
kuhusu waraka unaosambazwa nchi nzima ukidaiwa kutoka Makao Makuu.
Akihutubia maelfu ya
wananchi wa Nzega mjini akiwa ametokea eneo la Lusu ambako 'kulikuwa' na Mgodi
wa Resolute, Dk. Slaa amesema kuna waraka unasambazwa kwa viongozi wa wilaya
huku matapeli wa kisiasa wakiwalaghai viongozi hao kuwa umetolewa Makao Makuu
kutoka Ofisi ya Katibu Mkuu wa chama.
"Nimeletewa
taarifa hapa kuna watu wamepeleka fomu zao wakitaka watu watie saini kitu
kinaitwa petition...kwa sababu wanajua wanachofanya ni muendelezo wa uasi, juu
ya ile fomu hakujaandikwa kichwa cha habari chochote. Wanawadanganya watu kuwa
fomu hizo zimetoka Makao Makuu.
"Si kweli...Makao
Makuu kwa maana ya Ofisi ya Katibu Mkuu haijatoa kitu cha namna hiyo.
Wasidanganyike. Tunawapongeza wengi wao wameshtuka na wametupigia simu wakihoji
kitu hicho. Tunaujua mchezo unaotaka kufanyika. Lakini tunawaambia wahusika huo
ni uasi.
"Tunawaambia watu
wote waliopelekewa hizo barua zikiwa na fomu, fomu ambazo hazina kitu, lakini
wanaambiwa wajaze kwa kutia saini kwa sababu zimetoka taifa, wakatae. Mfano
watu wa Lindi na Mtwara ambao wametupigia simu baada ya kugutuka. Watu
wanasainishwa vitu wasivyovijua. Makao Makuu wala ofisi ya Katibu Mkuu
haijatuma kitu cha namna hiyo.
"Wamepeleka pesa
watu wanalipwa hela, najiuliza hizo hela malengo yake nini na nani amezitoa na
kwa maslahi ya nani. Hawa watu wanaochochea uasi ofisi yangu inaagiza wawe
makini sana, watajikuta matatani. Tunaujua mpango huo wote," alisema Dk.
Slaa huku akishangiliwa na umati wa watu kabla hajakaribisha maswali kutoka kwa
wananchi.
No comments:
Post a Comment