Akinwumi Adesina,
waziri wa kilimo Nigeria
Waziri wa Kilimo wa
Nigeria Akinwumi Adesina ametangazwa na jarida la Forbes Afrika kuwa mshindi wa
mwaka kutokana na mageuzi yake katika sekta ya kilimo.
"Ni mtu ambaye
yuko katika mwelekeo wa kuisaidia Afrika kujilisha," amesema mhariri wa
Forbes Africa,Chris Bishop.
Wachambuzi wa mambo
wanasema uchumi wa Nigeria kwa muda mrefu ulihodhiwa na mafuta ya petroli,
wakati kilimo kikipuuzwa, japokuwa kilimo kinategemewa na watu wengi.Bwana
Adesina amesema anataka kuwasaidia watu kutajirika kupitia kilimo.
"Lengo langu ni
kuwafanya watu wengi mamilionea, hata kuwa mabilionea, kutoka sekta ya kilimo
haraka iwezekanavyo," amesema katika hotuba ya kukubali tuzo hiyo.
Aliyu Tanko kutoka
Idhaa ya Hausa ya BBC, amesema Adesina ameanzisha uwazi zaidi katika usambazaji
na ugawaji wa mbolea, shughuli ambayo katika siku za nyuma iligubikwa na rushwa
kubwa.
Wanaigeria wengi
wanaishi katika dimbwi la umaskini, hususan katika maeneo ya vijijini.Waziri
pia amewataka raia wa Nigeria kulima zaidi mazao ya chakula, hasa zao la mhogo.
Mwezi Januari, Bwana
Adesina alitangaza mpango wa kuwagawia simu za mkononi wakulima milioni kumi
"ili kuleta mageuzi ya kilimo nchini humo," kwa hiyo wanaweza kupata
taarifa mpya za masoko.Simu hizo pia zinatumika kupata vocha za mbegu na mbolea.
Hata hivyo mwandishi
wetuamesema lengo hili bado halijafikiwa, akibainisha kuwa hakuna mtandao mzuri
wa simu katika maeneo mengi ya vijijini nchini humo.Chama kikuu cha upinzani
kilikosoa mpango huo kuwa ni "zoezi la kutafuta kura".
Bwana Adesina
aliwashinda baadhi ya wafanyabiashara wakubwa barani Afrika: Aliko Dangote na
Jim Ovia, pia kutoka Nigeria; Patrice Motsepe kutoka Afrika Kusini na Strive
Masiyiwa wa Zimbabwe.
Japokuwa nchi yao ni
moja ya nchi zinazozalisha mafuta kwa wingi duniani, wengi wa raia wa Nigeria
wanaishi katika hali ya umaskini mkubwa, hususan katika maeneo ya vijijini.
Bwana Bishop amesema
ana matumaini kuwa tuzo hiyo itawahamasisha watu wengi barani Afrika kupanda
mazao ya chakula chao wenyewe.
No comments:
Post a Comment