Utangulizi
Ukiitazama Nzega ya leo
si ile Nzega ya Miaka ya 90 ama ile ya miaka ya 70, alipozaliwa Mbunge wetu
Dkt. Hamisi Kigwangalla (Mb.), imebadilika sana, imekuwa kwa kasi sana; idadi
ya watu, magari na nyumba imeongezeka sana. Utoaji wa huduma zote muhimu
umezidiwa kasi na ukuaji wa mji. Changamoto zilizopo leo ni nyingi na nzito
sana. Kuna shida kubwa ya upatikanaji wa maji safi na salama, shule ni chache
na zinatoa elimu isiyokidhi ubora unaohitajika, viwanda hakuna ukilinganisha na miaka ya nyuma, migodi
midogo midogo iliyokuwa asili ya Nzega imefungwa na serikali, mvua zimepungua
kutokana na uharibifu wa mazingira hivyo uzalishaji wa mazao ya biashara na
kilimo umeathiriwa sana ukilinganisha na miaka ya nyuma, miundombinu ya
barabara imeongezeka kwa wingi haswa maeneo ya vijijini na mijini japokuwa bado
ni duni na haitoshi na pia huduma za kibenki ni duni na hazijawafikia wananchi
walio wengi kule vijijini.
Pamoja na mapungufu
haya Nzega inafaidika kwa kuwa kwenye nafasi nzuri kijiografia, kwamba ni
makutano ya barabara kuu ziendazo Kigoma, Kagera hadi Rwanda na Burundi na ile
inayokatiza kwenda Mwanza hadi Musoma na Tabora hadi
Mbeya. Kama
zikiunganishwa kwa lami, Nzega inaweza kuwa kituo muhimu kwa biashara. Pia
nafasi yake kijiografia imefanya Nzega iwe na mchanganyiko mzuri wa watu
kimakabila kiasi kwamba mchanganyiko huu unatoa fursa ya kuleta uzoefu na ujuzi
mbalimbali kutoka sehemu mbalimbali ambao unapafanya Nzega pawe mahala
palipochangamka (vibrant and dynamic).
Mwaka 2010, kwenye
uchaguzi Mkuu, Nzega ilifanya uamuzi sahihi wa kumchagua Mbunge mwanamapinduzi,
mwanamabadiliko na mpiganaji mahiri na makini, Dkt. Hamisi Kigwangalla (Mb.)
ambaye anajitahidi kupambana na changamoto hizi usiku na mchana pasi na kukata
tamaa ama kuchoka. Mafanikio ya kazi yake yanaonekana na siyo ya kutafuta.
Ifuatayo ni ripoti ya utekelezaji wa majukumu ya Mbunge wa Nzega, Dkt. Hamisi
Kigwangalla (Mb.) hadi kufikia Desemba 2013.
1. Hali ya Jimbo
Hali ya jimbo ni
shwari; amani, upendo na usalama umetamalaki japokuwa mpaka tunaandika taarifa
hii kuna malalamiko ya watu wa kijiji cha Mwanshina, ambako kuligundulika uwepo
wa dhahabu hivi siku za karibuni na kupelekea wananchi kujumuika pale kuanza
shughuli za uchimbaji; bahati mbaya sana wamezuiliwa na askari wa kutuliza
ghasia (FFU) waliopokea maelekezo kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Nzega.
Mazungumzo yanaendelea kujua ni kwa nini serikali imewazuia wananchi hawa ili
hatma ya mgodi huu ijulikane. Pili, kuna malalamiko ya wananchi wa kijiji cha
Ipala ambao wanadaiwa na serikali kupitia Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Nzega
kuvamia eneo la msitu wa hifadhi. Ufuatiliaji wa uhalali wa katazo la Mkuu wa
Wilaya ya Nzega lililoambatana na uvunjifu mkubwa wa haki za wananchi, ambapo
wamedumu toka kabla ya uhuru, unaendelea.
Ofisi ya Mbunge wa
Jimbo la Nzega imeendelea kuhudhuria shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo
harusi, misiba, mahafali za wanafunzi, harambee na pia kufanya ziara za kikazi
kijiji kwa kijiji kupitia ‘Operesheni Wafuate Watu’. Pia ahadi za Mbunge ama
wasaidizi wake kwenye maeneo mbali mbali zimekuwa zikitekelezwa – hadi sasa ni
zaidi ya asilimia 95 ya ahadi zote alizotoa mbunge zimetekelezwa ukiachilia
chache sana ambazo ni za siku za karibuni. Kuna ligi kubwa ya kiwilaya
inayofadhiliwa na Mbunge wa Nzega inaendelea katika hatua ya robo-fainali
kwenye tarafa nne za Wilaya ya Nzega – mshindi wa kwanza atapata ‘Kombe la
Kigwangalla’ na fedha taslim TZS 1,000,000, wa pili atapata TZS 500,000 na wa
tatu TZS 300,000. Timu zote zilizoingia nane bora zitazawadiwa seti moja ya
jezi kila timu.
Mbunge wa Nzega
anaendelea kupigana kuhakikisha azimio la Baraza la Madiwani la kuanzisha
Kampuni ya Benki Jamii ya Nzega (Nzega Community Bank Ltd - NCB) na Kampuni ya
Ujenzi ya Jamii ya Nzega (Nzega Community Construction Corporation Ltd -
NCCCL)linatekelezwa haraka. Tunatarajia mchakato huu utafanikiwa kutokana na
uwepo wa takriban TZS 2.3 bilioni zilizopatikana kutoka kampuni ya Resolute
Tanzania Ltd kama ushuru wa huduma (service levy) na ambazo zitatumika kama
mtaji wa kuanzia wa benki (TZS bilioni 1) na zinazobaki kwa ajili ya kununulia
mashine za kuchongea barabara na kuchimbia visima zitakazomilikiwa na
kuendeshwa na kampuni hizi mbili tofauti ambazo zinatarajiwa kuanzishwa kwa
ushirikiano baina ya Halmashauri, wanaushirika na wananchi wengine watakaopenda
kununua sehemu ya hisa za makampuni haya mawili.
2. Vipaumbele Vya Jimbo
2.1 Mapinduzi Kwenye Sekta ya Elimu Nzega:
(i.) Mbunge wa Nzega, Dkt. Hamisi
Kigwangalla, mpaka sasa kwa kufanya jitihada binafsi na kwa kutumia pesa za
mfuko wa jimbo (milioni 43) akishirikiana na Diwani, Mhe. Ramadhani Nchimani,
Kamati ya Maendeleo ya Kata ya Ndala, Serikali ya Kijiji cha Kampala na
wananchi kwa ujumla, ameanzisha ujenzi wa shule mpya ya ‘high school’ (kidato
cha tano na cha sita) pale Kampala, Ndala (Shule hii imepewa jina la Chief
Ngelengi High School); ujenzi unaendelea kwa kasi hivi sasa. Shule ya pili ya
High School itakuwa ni ile ya Chief Ntinginya, ambapo Mbunge wa Nzega Dkt. Hamisi
Kigwangalla, kufuatia makubaliano na Kamati ya Maendeleo ya Kata ya Nzega Mjini
chini ya Diwani na Mwenyekiti wake Mhe. Kizwalo Dominic waliazimia kuanzisha
ujenzi wa mabweni na madarasa ya ziada ili kuipandisha hadhi shule hii iwe ya
kidato cha tani na cha sita. Shule ya tatu ya High School inamaliziwa kujengwa
Kata ya Puge, Tarafa ya Puge kwa ushirikiano wa Ofisi ya Mbunge (ambayo imetoa
sh milioni 13), Diwani Mhe. Alex Nyassani, Serikali ya Kijiji cha Upungu na
wananchi kwa ujumla (ambao walianzisha majengo hayo); pia Halmashauri ya Wilaya
tayari, kwa ushawishi wa Mbunge wa Nzega na Diwani wa Kata ya Puge, imetenga
fedha taslimu sh milioni 28 kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa shule hiyo. Shule
ya Nne ya High School inamaliziwa kujengwa kule Kata ya Lusu (pale Hamza Azizi
Ali Sekondari) na wawekezaji wa mgodi, Kampuni ya Resolute Tanzania Ltd,
kufuatia jitihada za kiufuatiliaji na ushawishi wa Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla
(Mb.) na Mhe. Said Mgalula (Diwani, Lusu) wakishirikiana na wananchi, kwamba ni
lazima mgodi ujenge miradi ya maendeleo ya jamii kabla haujafungwa. Ni
matarajio yetu kwamba shule hizi zitakamilika na kuanza kudahili wanafunzi
kabla ya mwaka 2014 kuisha. Tunawaomba wananchi wote kwa ujumla, wadau
mbalimbali wa maendeleo na serikali tutimize wajibu wetu, tumuunge mkono Mbunge
wetu tulete mapinduzi ya kielimu Nzega.
(ii.) Mbunge wa Nzega, Dkt. Hamisi
Kigwangalla, akishirikiana na shirika lisilo la kiserikali la PeerCorps Trust
Fund ameweza kuanzisha mpango wa kusomesha watoto yatima na wanaotoka familia
zenye kipato duni, mfuko huu unaoitwaHamisi Kigwangalla Scholarship Fund
ulianzishwa mwaka 2008 na umeendelea kusomesha watoto na kutoa misaada
mbalimbali ya kielimu. Mpaka sasa zaidi ya watoto 576 wamefaidika na mpango
huu. Na kila kata kuna wanafunzi 10 kutoka katika makundi haya wanalipiwa ada
chini ya mpango huu. Japokuwa mfuko unakumbana na changamoto nyingi ikiwemo
kupata maombi mengi zaidi ya uwezo wa mfuko na kuna baadhi ya kata mpaka sasa
mfuko haujaweza kupata fedha za kulipa ada kwa baadhi ya wanafunzi, japokuwa
Mhe. Mbunge anawataka walimu, wazazi/walezi na viongozi wa Kata hizo wawe
wavumilivu na kwamba ada hizo zitalipwa kabla watoto hao hawajahitimu kwa kuwa
majina yao tunayo na yaliishapitishwa kufaidika na mpango huu.
(iii.) Mwezi Januari mwaka 2014 Mbunge wa
Nzega, Dkt. Hamisi Kigwangalla, atauanza mwaka kwa kuendelea kugawa vitabu 100
vya Kiada na 50 vya ziada kwenye shule zote za Sekondari za Kata za Jimbo la
Nzega pamoja na Kompyuta kwenye shule 5 za sekondari kama ambavyo amekuwa
akifanya toka achaguliwe kuwa Mbunge wa jimbo hili.
(iv.) Mbunge wa Nzega, Dkt. Hamisi
Kigwangalla, ameanzisha tamasha la utamaduni wa watu wa Nzega litakalokuwa
likifanyika kila mwaka mjini Nzega. Tamasha hilo ambalo linaitwa Mtukwao
Festival (www.mtukwao.org) litakuwa ni kivutio cha watu na kuleta fursa ya
biashara kwa wakazi wa Nzega, na sehemu ya kuitangaza Nzega na utamaduni wake
kwa wageni, tayari limepata usajili wa serikali na maandalizi yanafanyika kulizindua
mnamo Julai 2014 kwa mara ya kwanza, baada ya mipango ya kulizindua Julai 2013
kama ilivyotangazwa hapo awali kushindikana.
(v.) Mbunge wa Nzega, Dkt. Hamisi
Kigwangalla, ameanzisha ujenzi wa chuo binafsi mjini Nzega eneo la Uchama kitakachokuwa
kinatoa wahitimu kwenye fani za Uganga, Uuguzi na Ualimu kwa ngazi za Vyeti na
Stashahada ili kuongeza nguvu kazi kwenye shule za sekondari za kata, zahanati
na vituo vya afya. Malengo ni kusomesha bure walau wanafunzi watano - kwenye
kila kozi, wasio na uwezo, mbali na wale wanaojilipia, kwa makubaliano ya
kuhakikisha wanaajiriwa kwenye wilaya ya Nzega kwa kipindi kisichopungua miaka
mitano. Hii itaongeza idadi ya watumishi kwenye huduma muhimu kwa wananchi na
pia uwepo wa chuo utakuza fursa za kiuchumi na ukuaji wa taswira ya mji wa
Nzega. Tunatarajia chuo hiki kitakamilika na kuanza kudahili wanafunzi mwaka
2014 Mwezi Septemba.
2.2 Kuendesha Harakati za Kupigania Haki na Usawa
kwa wanaNzega: Mbunge wa Nzega, Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla, akishirikiana na
wananchi wa Nzega, madiwani na watendaji wa halmashauri ameongoza mapambano ya
kudai haki za Nzega dhidi ya wawekezaji wa Mgodi wa Golden Pride Project,
kampuni ya Resolute Tanzania Ltd, na kufanikiwa kupata mafanikio yafuatayo:
mgodi umekubali na tayari umelipa sh bilioni 2.34 kama ushuru wa huduma
(service levy) kwa halmashauri ya wilaya ya Nzega, bado kuna madai ya sh
bilioni 4 za ushuru wa huduma yanayoendelea kufuatiliwa, ambazo ni malimbikizo
ya ushuru huo toka mgodi uanzishwe takriban miaka 14 iliyopita; amefanikiwa
kuishawishi serikali kuwa wananchi waliopoteza mali zao kutokana na uharibifu
uliofanywa kupisha mgodi wana haki ya kifuta jasho na sasa serikali inaungana
na Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla kuwabana wawekezaji waanzishe mfuko wa
kuwahifadhi wananchi hao; na jambo kubwa la tatu ni kwa kutumia nguvu ya umma
kushawishi wawekezaji watekeleze ahadi za kujenga miradi ya maendeleo Nzega
(Kituo cha Afya Lusu, Maabara kwenye sekondari 10 n.k.). Mbunge wa Nzega
ataendelea kushawishi vikao vya halmashauri na kusimamia utekelezaji wa miradi
itakayowagusa wanaNzega wengi zaidi, kama vile kuanzisha benki ya jamii ya watu
wa Nzega ambayo itatoa mikopo kwenye SACCOS za kila kata, kununua mitambo yetu
wenyewe ya kuchimbia visima kwenye kila kijiji, kujenga soko jipya na stendi
mpya kubwa ili kukuza fursa za biashara ndogondogo kwa wananchi n.k. Mhe.
Mbunge amekuwa akipigana bega kwa bega na wananchi wa Kijiji cha Mwabangu
kuhakikisha wanapata haki ya kupatiwa leseni yao iliyopokwa kinyemela na wajanja
wachache kwa faida yao ama fidia ya ardhi ya mgodi wa wachimbaji wadogo wadogo
wa Isungangwanda.
2.3 Kuwezesha Wananchi Kushiriki Shughuli
Mbalimbali za Kukuza Kipato Chao: Mbunge wa Nzega, Mhe. Dkt. Hamisi
Kigwangalla, amefanikiwa kuleta mapinduzi ya kijani kwenye kilimo cha zao la
pamba na zao la alizeti kupitia uhamasishaji wa kampuni ya MSK Solutions Ltd
ambayo inatoa mbegu bora, pembejeo, zana za kilimo, elimu ya kilimo bora na
uwezeshaji wa wagani vijijini, soko la uhakika la mazao hayo na ujenzi wa
maghala ya kuhifadhia mazao vijijini (Imekamilisha ujenzi wa maghala kule
Ndekeli (Tarafa ya Puge), Igalula (Tarafa ya Mwakalundi), Nhabala (Tarafa ya
Bukene) na imeanza ujenzi wa ma-godown mapya kule Nhobola (Tarafa ya Nyasa) na
Usongohala (Tarafa ya Bukene). Mafanikio ni kuongezeka kwa wakulima wa pamba
kutokea wakulima 355 mwaka 2008 hadi kufikia wakulima 24,000 wa pamba mwaka
2012 na kufanya idadi ya kilo za pamba zilizovunwa kufikia takriban milioni 6
kutoka kilo 20,000 mwaka 2008. Pia idadi ya wakulima wa alizeti imeongezeka
kutoka wakulima 400 mwaka jana hadi kufikia 3500 mwaka 2013.
Makampuni ya wanunuzi
wa pamba yameongezeka kutoka kampuni moja ya MSK na kuwa manne hivi sasa – hali
inayoleta ushindani kwenye soko na hivyo kupandisha bei zaidi kwa faida ya
mkulima. Japokuwa kampuni ya MSK Solutions Ltd imeamua kuacha kuhamasisha pamba
na kujikita zaidi kwenye alizeti itaendelea kukumbukwa kwa kutia chachu
uhuishaji wa kilimo cha zao hili kilichokuwa kimekufa.
Mipango inaendelea
kuwashawishi wawekezaji wajenge viwanda vya kuchambua pamba na kukamua mafuta
ya kula kutokana na alizeti ya Nzega, tayari halmashauri ya Nzega imeazimia
kutenga viwanja 10 kwenye eneo maalum la kujenga viwanda. Pia Mbunge wa Nzega
amewezesha wananchi kujiunga katika vikundi vya ushirika wa SACCOS vipatavyo 9
na yupo kwenye harakati za kuvijengea uwezo vifanye kazi za kukuza uchumi kama
vile kilimo, mifugo ya kuku kwa kuzalisha vifaranga na mayai, na shughuli za
ufundi kwa vijana. Mbunge wa Nzega amegawa mashine mbili kwenye SACCOS ya
vijana nay a wazee kwa ajili ya kuangulia vifaranga. Ili kuhakikisha chama kinakuwa
mstari wa mbele katika kuhamasisha shughuli mbalimbali za maendeleo vijijini,
Mbunge wa Nzega akishirikiana na mwenzake wa Bukene wamegawa mbegu za alizeti
kwenye kila kata. Pia Mbunge wa Nzega amegawa pikipiki 10 kwenye kata 10 ili
kuweka urahisi zaidi wa kufikisha huduma za ushauri wa maendeleo kwa wakulima
vijijini.
2.4 Ujenzi wa Miundombinu Nzega: Mbunge wa Nzega,
Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla, ameweza kushawishi vikao mbalimbali vya maamuzi
na kuhakikisha azimio la kujenga barabara za lami Nzega Mjini linafanikiwa,
hivi sasa tayari bajeti imetengwa kwa ajili ya kutekeleza hilo kwenye mwaka wa
fedha wa 2013/14; pia kufunga mataa ya kuangaza mji mzima wa Nzega. Mbunge wa
Nzega pia kupitia mfuko wa Jimbo amejenga daraja korofi na lililosahaulika kwa muda
mrefu la Butandula, na sasa anatafuta namna ya kuhakikisha pia daraja lingine
la Nhobola nalo linajengwa, tayari ametenga sh milioni 8 za mfuko wa jimbo
kutekeleza hilo.
Mradi wa barabara ya
Nzega – Tabora kwa kiwango cha lami – Mbunge wa Nzega kwa kutumia nafasi yake
kama Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Tabora, amekuwa mstari wa
mbele kuhakikisha serikali inaleta fedha za kukamilisha mradi huu ndani ya muda
uliopangwa na pia kusimamia kuhakikisha barabara hiyo na nyingine za mkoa wa Tabora,
zinajengwa kwa viwango vya ubora unaostahiki, na wananchi wanapata ajira na
kulipwa fidia ya mali zitakazoathiriwa na utekelezaji wa mradi huu.
Pia Mbunge amehakikisha
barabara korofi kama za kutoka Mbagwa – Nkiniziwa, Busondo – Ndekeli, Busondo –
Mwakashanhala zinaingia kwenye bajeti ya ujenzi mwaka huu wa fedha 2013/14 na
kuhakikisha zinajengwa, pia barabara nyingine muhimu kama za Muhugi –
Mizibaziba – Ndekeli – Ndala zinaingizwa kwenye bajeti, lengo likiwa ni
kuhakikisha Nzega inakuwa na mtandao mzuri wa lami mahala pote. Mhe. Dkt.
Hamisi Kigwangalla (Mb.) amefanikiwa kuhakikisha mradi wa kupeleka umeme Ndala
kutoka Nzega unatekelezwa kwa viwango vya ubora unaofaa, na sasa anahangaika
kuhakikisha pia maeneo ya Mbogwe, Wela, Miguwa, na yale ya Usagali, Kaloleni
hadi Mirambo Itobo nayo yanapata mradi wa Umeme. Tayari maombi yake yameingizwa
kwenye orodha ya miradi ya Umeme Vijijini (REA Phase II) na hivyo maandalizi ya
awali ya upembuzi yakinifu yataanza muda wowote kuanzia sasa. Sambamba na jitihada
hizi, Mbunge amefanikiwa kuishauri na hatimaye kuishawishi halmashauri ya Nzega
kuanzisha kampuni ya ujenzi (NCCCL) na kuinunulia mitambo ya kuchongea
barabara, mpango ambao upo kwenye hatua za utekelezaji.
2.5 Upatikanaji wa Maji Safi na Salama Nzega:
Baada ya kutoridhishwa na namna miradi ya maji ya benki ya dunia na ile ya
serikali inavyosuasua, Mbunge wa Nzega, Dkt. Hamisi Kigwangalla, ameshauri na
hatimaye kuishawishi Halmashauri wanunue mitambo ya kuchimba visima na kuiweka
chini ya usimamizi wa kampuni ya ujenzi Nzega (NCCCL) ili kuondoa yale matatizo
kwamba mkandarasi amelipwa achimbe kisima kimoja akikosa maji basi na pesa ya
serikali ndiyo imeishaliwa. Pesa za kununulia mitambo hiyo zitatokana na mapato
yaliyopatikana kutokana na ushuru wa huduma uliolipwa na kampuni ya Resolute.
Tukiwa na mitambo yetu tutahakikisha tunachimba kisima na maji yanapatikana
kwenye kila kijiji bila shida ndipo twende kijiji kingine. Pia Mhe. Mbunge
amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kuja
Mkoa wa Tabora unaanza kutekelezwa – na kwa sasa hatua ya utafiti wa awali
ilishamalizika na tunatarajia upembuzi yakinifu utafanyika mwaka huu na pengine
mwakani kuanza kutekelezwa, ukizingatia hii ni ahadi ya Mhe. Rais Dkt. Jakaya
Kikwete.
2.6 Upatikanaji wa Huduma Bora za Afya kwa Umma:
Mhe. Mbunge, Dkt. Hamisi Kigwangalla, ameamua kuanzia mwaka 2014 ataweka ratiba
maalum ya kutumia taaluma yake ya udaktari kutibu wagonjwa kwenye vituo mbali
mbali vya afya Nzega. Pia ameandaa mkakati kabambe wa kuleta madaktari bingwa
wanaoruka (flying doctors) kwa ajili ya kuweka kambi ya tiba maalum mara mbili
kwa mwaka kwa ajili ya wananchi wa Nzega. Kwa kushirikiana na madiwani wenzake
wa halmashauri ya Nzega wamefanikiwa kuhakikisha vituo pamoja na nyumba za
walimu zilizoanza kujengwa na wananchi vinamaliziwa chini ya Mpango wa
Maendeleo ya Afya ya Msingi – tayari bajeti imetengwa kumalizia vituo vyote
mwaka 2013/14, na anaendelea kuhamasisha vijiji vingine ambavyo havijaanza
kutekeleza mpango huu vianze mara moja ili tubaki tukitafuta namna ya kupambana
na chamngamoto nyingine za watumishi, vifaa na madawa.
N.B: Kuna mambo mengi
yanayofanyika Nzega kwa ushawishi wa Mbunge na Madiwani, yakitekelezwa na
serikali kutokana na maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM, mwaka 2010 – 2015,
lakini si yote yaliyoripotiwa hapa.
Taarifa hii imetolewa
na Ofisi ya Mbunge, Jimbo la Nzega
Mhe. Dkt. Hamisi A.
Kigwangalla (Mb.)
No comments:
Post a Comment