JAMHURI YA MUUNGANO WA
TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA
NDANI YA NCHI
JESHI LA POLISI
TANZANIA
Mnamo tarehe 18/12/2013
majira ya saa tatu asubuhi katika kata ya Malinyi, tarafa ya Malinyi, wilaya ya
Ulanga, mkoani Morogoro, kundi la watu kutoka maeneo mbalimbali kijijini hapo
walivamia kituo cha Polisi Malinyi kwa
lengo la kutaka kuwatoa kwa nguvu watuhumiwa 4 waliokuwa wamekamatwa kwa tuhuma
za mauaji.
Katika jitihada za
kuhami kituo, askari polisi walitoa tahadhali mbalimbali za kuwataka wananchi
hao watawanyike ikiwemo
kupiga mabomu ya machozi, lakini wananchi hao
waliendelea kukaidi amri hiyo. Katika purukushani hizo za askari kutetea kituo
na wavamizi kuendelea kuharibu mali za kituo ikiwemo kukichoma moto, wananchi 3
walipoteza maisha na wengine 3 walijeruhiwa.
Kufuatia tukio
hilo, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini,
IGP Said Mwema, ametuma timu maalumu ikiongozwa na Kamishina wa Operesheni
na Mafunzo (CP) Paul Chagonja kutoka Makao Makuu ya Polisi kwenda
kuongeza nguvu katika Operesheni ya kuwasaka na kuwakamata wote
waliohusika na tukio hilo, ili wafikishwe katika mkondo wa sheria haraka.
Jeshi la Polisi linalaani
vikali tukio hilo linaloashiria vitendo vya vurugu na uvunjifu wa amani,
tukio ambalo limesababisha vifo na majeruhi pamoja na kujenga hofu miongoni mwa
jamii.
Aidha, IGP Mwema ametoa
wito kwa wananchi wa mkoa wa Morogoro hususani wilaya ya Ulanga kata ya
Malinyi, kuwa watulivu na kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi
wakati uchunguzi ukiendelea, mtu yeyote mwenye taarifa za wahalifu hao anaombwa kutoa taarifa kwenye
namba ya simu ifuatayo 0754 78 55 57 au katika kituo chochote cha Polisi, ili
wahalifu hao waweze kukamatwa na kufikishwa mahakamani.
Imetolewa na:-
Advera Senso-SSP
Msemaji wa Jeshi la
Polisi.
No comments:
Post a Comment