Yaya Toure aliteuliwa
mara tano kuwania tuzo hili lakini akafanikiwa kushinda mwaka huu
Yaya Toure ametangazwa
mshindi wa tuzo ya BBC ya mwaka 2013 ya mchezaji bora zaidi wa soka barani
Afrika.Mchezaji huyo ana
umri wa miaka 30.
Mchezaji huyo wa Ivory
Coast, na ambaye pia ni kiungo wa klabu ya Manchester City ya Uingereza, na
ambaye jina lake limekuwepo kwa miaka minne iliyopita katika orodha ya
wachezaji wanaowania tuzo, aliwashinda Pierre-Emerick Aubameyang, Victor Moses,
John Mikel Obi na Jonathan Pitroipa, katika kuibuka mshindi.
Orodha fupi ya
waliowania tuzo hiyo ilitayarishwa na wataalamu 44 wa soka kutoka kote barani
Afrika, na wakizingatia hasa maarifa ya mchezaji, kiufundi, ushirikiano na
wenzake katika timu, na kwa kucheza mchezo safi na kwa haki.
Kisha, kupitia idadi
kubwa kabisa kuandikishwa kwa wapiga kura, mashabiki waliweza kushiriki katika
shughuli hiyo katika mtandao, au kupitia ujumbe wa simu ya mkononi.
Mashabiki hao wameamua
kwamba Toure ndiye bora zaidi, kwani katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita,
raia huyo wa Ivory Coast alicheza kwa bidii, kuonyesha mchezo wa kasi, ubunifu,
na vile vile kwa kufunga magoli.
Ingawa mwaka 2013
ulikuwa ni wa ufanisi kwa Toure hasa kwa kupata vikombe, hakuweza kuisaidia
nchi yake, wala klabu, kupata kombe lolote lile, lakini bado alionyesha kiwango
cha hali ya juu katika mchezo.
Baada ya kuvunjika moyo
kwa kushindwa kuutetea ubingwa wao wa ligi kuu ya Premier wa mwaka 2012
akiichezea Manchester City, Toure alirudi uwanjani akijizatiti, na kuimarisha
mikwaju yake ya free-kick.
Alitumbukiza wavuni
bao, kwa mpira wa kupinda, katika siku ya kwanza ya msimu mpya wa ligi kuu ya
Premier, wakati timu yake ilipocheza na Newcastle, na akarudia hayo hayo katika
mechi iliyofuata wakati Hull walipowatembelea katika uwanja wao wa nyumbani.
Toure amefunga magoli
manne ya kupanga kwa makini shambulio, na hayo yakiwa ni kati ya magoli saba
kwa jumla aliyoweza kuifungia klabu ya Man City msimu huu.
Kufikia sasa, mwaka huu
wa 2013, Toure ametumbukiza wavuni jumla ya magoli 12; ya klabu na vile vile ya
nchi yake, na hiyo ni rekodi nzuri sana kwa mchezaji wa kiungo cha kati.
Mbali na ustadi huo
katika kumalizia, Toure ni kiongozi bora katika timu, na maarifa yake
yameiwezesha City kufikia sasa kuwa katika nafasi ya nne katika ligi kuu ya
England.
Aliisaidia kikamilifu
nchi yake ya Ivory Coast kufuzu kwa michuano ya Kombe la Dunia ya mwaka ujao
itakayofanyika nchini Brazil.
Timu yake ya Tembo, The
Elephants ilihitaji kuusahau mwanzo mbovu hapo awali katika kampeni yao ya
michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika, na walipoondolewa katika robo fainali
na Nigeria, ambao hatimaye waliibuka mabingwa, na Toure akiwapa matumaini ya kufanya
vyema baadaye.
Nje ya uwanja, Toure
ameongoza vita dhidi ya ubaguzi wa rangi katika soka, hasa baada ya matusi
kuelekezwa kwake katika mechi ya ligi ya klabu bingwa dhidi ya CSKA Moscow,
mwezi Oktoba, na akionyesha moyo wa uvumilivu na wa kimichezo unaostahili
uwanjani.
Tukio kama hilo
linaweza kumvunja moyo mchezaji asiyejiamini, lakini Toure ameendelea kuwa
mchezaji wa kipekee tangu wakati huo.
Na katika mwaka wa tano
baada ya jina lake kupangwa katika orodha ya wachezaji wanaowania tuzo,
hatimaye Toure ametajwa kama mshindi wa tuzo ya mchezaji bora zaidi wa soka
barani Afrika.
No comments:
Post a Comment