Thursday, December 12, 2013

MARA ZOTE TUMEKUA TUKIONA HAIWEZEKANI MPAKA PALE TUNAPOONA WENGINE WAMEFANYA NA IMEWEZEKANA.




Ziara ya kutembelea kiwanda nchini CHINA kwa ajili ya kukubaliana utaratibu wa uzalishaji-Oct 2013
Hyasintha B. Ntuyeko managing director of Kasole Secrets company ltd, leo akisheherekea miaka 3 ya biashara yake.
Nilianza biashara 6 Dec 2010 kwa mtaji wa shilling 60,000/= ambao nilipatiwa na Aunt yangu (Victoria Isangu) Mara tuu baada ya kumaliza chuo.

Huu ndo ulikua mwanzo wa biashara, nilianza kufuata mzigo mwenyewe Mombasa- 2011

Ni kweli kabisa baada ya masomo ya chuo nilitumia muda wangu mwingi kuangalia series (kipindi kile ilikua prison break) huku nikisubiri muda ufike nirudi nyumbani kusubiria ajira.

Kwa kweli sikuwahi kuota kufanya biashara, ndoto zangu zilikua kufanya kazi katika makampuni makubwa ya mawasiliano huku nikiwa nimeshajipangia kiasi cha mshahara ambao ningelipwa. Sasa hili wazo la biashara nililopewa na Aunt Vicky sikujua jinsi ya kulianza.

Aunt Vicky aliniambia badala ya kukaa bure unaonaje kama ukiwa unauza hizi bidhaa ukajipatia hela kidogo za matumizi? Ni kamuuliza sasa hii biashara inafanywaje? Akaniambia Ongea na kila mtu unayekutana nae, hao ndo wateja wenyewe. 

Nikakubaliana nae, akanilipia 60,000/= nikachukua pads( hizi pads zilikua zikitengenezwa na mmea unaitwa leonorus) na vipodozi vingine vya gharama hiyo, Nikaondoka kuelekea nyumbani (nilikua nikikaa na rafiki yangu kipindi hicho wakati nasubiria kurudi nyumbani).

Hii ndio ofisi niliyoifungua na kuachana na biashara za kuzunguka barabarani- July 2011

Hiyo siku nilirudi nyumbani nikamuonyesha rafiki yangu akaniambia fanya ni kitu kizuri, kesho yake nilikaa tuu nyumbani sikwenda popote, siku inayofuata nikaamua kutoka kujaribu kuuza bidhaa zangu,  nilianza na mwenge na nilitembea kwenye maframe ya mwenge na kuongea hata na wapita njia, siku hiyo nilipata tsh 20,000/= Kwa kweli nilifurahi mnoo, kwanza nilishangaa inawezekanaje siku moja tuu niweze kuzalisha tsh 20,000/=? Wakati nilikua na 20,000/= nimeihifadhi kwa muda wa mwezi mzima kwa ajili ya kuitumia kama nauli muda utakapofika wa kurudi nyumbani, sio siri nilikua siwezi hata kutoa sadaka kanisani nikihofia ikipugua sitaweza kuongezea. Leo siku moja tuu nimepata 20,000/=? yaani nilijiona tajiri sana. Sasa Nguvu ya kuifanya hii biashara ikapatikana

muonekano mpya wa ofisi yangu July 2012

Watu walioniagiza niwaletee bidhaa kesho yake walikua wengi hivyo nikampigia Aunt Yangu kumueleza kua nina oda za watu na hela iliyopo mkononi haitatosha, akaniongezea tsh 90,000/= nikafuata kununua mzigo kwa rafiki yake (Mama Mbise) kisha nikaendelea na biashara, kwa kweli ilikua nzuri sana, nilizidi kutembea na kuziuza vyuoni pia. Nilipata wateja wengi sana kiasi Mama Mbise (rafiki yake aunt yangu) hakuweza tena kuniuzia mzigo, akanielekeza niwe ninaufuata mwenyewe Mombasa-Kenya.
VIKWAZO

Binafsi hua ninavichukulia Vikwazo/changamoto kama ni shule pekee ya mjasiliamali, hakuna njia nyingine yeyote ambayo mjasiliamali anaweza kuongeza ujuzi na uzoefu kama hata kumbana na vikwazo vyovyote katika biashara yake.
Kikwazo cha awali nilichokumbana nacho ni kutoka kwenye kikundi cha sala (fellowship) nilichokua ninasali , ninapenda kusali hivyo hua ninajishughulisha na shughuli zozote zinazonifanya niwe karibu na Mungu.

Niliwashirikisha biashara baadhi ya marafiki zangu niliokua ninasali nao kikundini, walivutiwa na wenyewe wakawa watumiaji, muda mchache nikaona wameacha kutumia na kila nikiwauliza hawakunipa majibu ya moja kwa moja, siku moja mmoja wa niliowapa bidhaa zangu akaniambia, unajua Hyasintha tumeacha kutumia bidhaa zako kwasababu zinahusiana na FREEMANSON, eeeh! Nilishangaaa sana, nikamuuliza ili anieleweshe, akanipa Maelezo ambayo kichwani kwangu hayakukubalika hata kidogo, nikamwambia sawa, we acha kutumia na kuifanya hii biashara ila acha mi niifanye siku moja mtanitumia mimi kama mfano.

Siku chache baadae viongozi kadhaa wa fellowship waliniita kunikanya kuhusu hii biashara yangu na kunitaka nimuombe Mungu anitafutie kazi nzuri, kwa kweli sikuwaelewa kabisa nikaamua kuendelea na biashara kwani niliamini kama mimi pia ninasali basi ninauwezo wa kugundua la Mungu na la shetani.

Nikiwa chuo nakumbuka kuna mgomo wa wafanyakazi uliwahi kutokea, RAIS alihutubia akasema
“ AKILI ZA MGAYA CHANGANYA NA ZA KWAKO” huu msemo niliupenda sana, hivyo hata katika kikwazo hiki ulikua ukinifariji mno. Ni kweli kama nisingeamua kwa busara, ndoto yangu ingezimikia pale.

 Baada ya kunogewa na biashara nilisahau kabisa swala la kutuma barua za maombi ya kazi, hivyo kujikuta ninaingia matatani na familia, Ndugu na jamaa walinilaumu kwa kutotafuta kazi na kufanya biashara isiyoeleweka, nina mshukuru sana Mama Mbise (Rafiki wa Aunt Yangu) ambaye yeye alikua ni mshauri wangu mkuu na alinitia moyo mno nikaweza kuishinda hii changamoto. 

Hivyo katika biashara yoyote tunahitaji mshauri ambaye ataweza kutuelekeza njia na kutushika mkono, ni vyema kuchagua mshauri sahihi, si kila mtu anaweza kukushauri katika biashara yako, wengine wanaweza kukufanya ukate tamaa kabisa na kupoteza mwelekeo.
Biashara yangu ilienda vizuri sana na ilipanuka, nikatoka hatua moja kwenda nyingine,  kutoka mmachinga hadi kufungua ofisi na kukaa mahali pamoja sasa.

nikiwa Nairobi kukubaliana na hiyo kampuni kuhusu kupata mzigo moja kwa moja Tanzania, dada aliyevaa hijabu ni rafiki yangu, waliobaki ni administration ya hiyo kampuni. NAIROBI-KENYA 2011

Hapa sasa nikapambana na changamoto nyingine, kampuni iliyokua ikiniuzia bidhaa kutoka Nairobi wakaanza usumbufu wa kutoleta bidhaa, wanaweza chelewesha bidhaa kwa zaidi ya miezi mitatu hadi minne na mimi ninawateja na sina biashara nyingine ninafanya hapa mjini ni hiyo tuu. Nikaanza kuingia ugomvi na wateja kwa kushindwa kuwapa bidhaa kwa wakati. Niliudhika sana, Changamoto hii ilinifanya nikae chini nifikirie na mimi kua na kitu changu mwenyewe na si kutegemea watu wengine ambao sijui ghala lao lina ukubwa gani. Hapo ndipo wazo la pads za mkaa wa mianzi lilipozaliwa,

Nilitumia muda wangu mwingi kusoma na kutafuta kwa kina kuhusu mkaa wa muanzi na vipi unahusika na afya ya uzazi ya mwanamke, nilipanda milima na mabonde kuhusiana na jambo hili bila

kukata tamaa kamwe. Baada ya kujiridhisha nilifungua kampuni yangu  ya KASOLE SECRETS, 18TH Feb 2013.

 


Kasole ni jina langu nililopatiwa na Baba yangu likiwa na maana ya “kitu kizuri” na niliweka neno “Secrets” likiwa na maana ya siri, Neno Siri linatokana na historia yangu hasa jinsi nilivyoanza kufanya biashara, hivyo “Kasole secrets” Inatafsiriwa kama “SIRI NZURI” Siri zilizopo katika kujiamini, kua na msimamo, kuthubutu kufanya jambo bila kusita, kujituma, kutodharau fursa na kutokata tamaa.

Hapa nikiwa katika moja ya supermarket nikizinadi pads zangu, sikua bado na uwezo wa kutengeneza sare yangu, lakini sikukata tamaa

Glory Girl pads ni pad bora ya afya iliyowekwa mkaa wa muanzi wenye kufyonza sumu, kuimarisha kinga ya kizazi na mzunguko wa hedhi, kukuondolea maumivu makali ya tumbo na viungo kabla na wakati wa hedhi.

nikiwa kwenye maonyesho ya sabasaba JULY-2013

Mpaka sasa nimeweza kusambaza zaidi ya sehemu 40 jijini Dar na hata nje ya Dar kwa mikoa kama KILIMANJARO, ARUSHA, MWANZA, MBEYA NA DODOMA.
Hapa nikiwa ninafundisha kina mama juu ya pads za muanzi.  FEB 2013

picha baada ya kufundisha kikundi cha wajasiliamali juu ya pads za Muanzi, MARCH 2013
Tembelea page yetu ya facebook ya Amani bamboo uweze kupata taarifa zaidi

NINAPOKUA NIKIADHIMISHA MIAKA HII 3, NINAPENDA KUSEMA..........

Kila kitu kinawezekana kufanyika kama kweli tukiweka nia, Hatukuamini kama South Afrika ingeweza kutawaliwa na waafrika wenyewe, lakini NELSON MANDELA alituaminisha kua inawezekana baada ya yeye kuitawala South Afrika, Hatukuamini kama Rais mwenye asili ya Kiafrika   angeweza kuingoza Marekani mpaka OBAMA aliposhinda Urais, pengine hatuamini vitu vingi kama sisi binafsi tunaweza kufanya na hivyo kutothubutu kujaribu kabisa.

Tunaweza kuleta mabadiliko na kufanya maajabu, tunaweza kuishi maisha yoyote tunayoyataka, tunaweza kua wafanya biashara wakubwa hapa Duniani, njia rahisi nikufikiria nini Ufanye na ukifanye vipi, swala la mtaji utalifikiria baadae baada ya kupata majibu ya nini ufanye na ukifanye vipi.

Binafsi ninawaahidi kipindi kingine nitakapokua ninasheherekea miaka kadhaa ya Glory Pads nitakua nimeweza kuifanya glory pads kua international brand..........

nikiwa nimevalia vizuri kabisa tayari kuingia ndani kabisa katika mitambo yao ya uzalishaji ili kuweza kuona ni jinsi gani wanafanya kazi- CHINA NOV 2013


 INAWEZEKANA JAMANI..... Tembelea ukurasa wetu wa facebook uitwao amani bamboo

No comments:

Post a Comment