Tuesday, May 15, 2012

Siku Ya Familia Duniani


                   TAARIFA YA MAADHIMISHO YA SIKU YA FAMILIA DUNIANI TAREHE 15 MEI 2012





Siku ya Familia Duniani huadhimishwa kila mwaka tarehe 15 Mei na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa.  Maadhimisho hayo yanatokana na tamko la Baraza la Umoja wa Mataifa Na. 47/257 la tarehe 20 Septemba, 1993, linaloidhinisha kuwa na Siku maalum kwa ajili ya familia. Tanzania ni moja ya wanachama wa Umoja wa Mataifa hivyo huungana na nchi nyingine kila mwaka kuadhimisha siku hii. Mwaka huu maadhimisho haya yatafanyika kimkoa.
Madhumuni ya Siku ya Familia Duniani ni kuhamasisha, kuhimiza, kuelimisha na kutanabahisha jamii kuhusu umuhimu wa familia katika jamii kwa nia ya kuchukua hatua zinazopasa ili kuziimarisha na kuziendeleza. 
Kauli mbiu ya Siku ya Familia mwaka huu ni: “UWAJIBIKAJI SAWA KATIKA MAJUKUMU: MSINGI WA FAMILIA BORA”. Kauli mbiu hii inalenga kuhamasisha, kuhimiza, kuelimisha familia na jamii kugawa muda wa kazi za kiuchumi na kuacha muda wa kutosha kutekeleza majukumu ya familia, hasa ya kulea na kukaa na watoto/familia hivyo kujenga umoja, uadilifu na upendo kwa familia. Ushindani uliopo katika soko huria ni changamoto kwa wazazi wa kizazi cha sasa  kutopata muda wa kutosha kuwa na familia.  Aidha, majukumu yanaongezeka siku hadi siku ambayo husababisha wazazi/walezi kufanya kazi siku zote za wiki na hata usiku, hatimaye kupunguza muda wa kukaa na familia hasa watoto wao na hivyo kusababisha kutokuwepo kwa uwiano wa kazi na majukumu ya malezi.
Pamoja na kwamba tunatakiwa kufanya kazi kwa bidii ili kukidhi mahitaji ya familia, inabidi kuwianisha muda wa kufanya kazi na kukaa na familia ili watoto wapate malezi stahiki.
Familia nyingi za Kitanzania zinakabiliwa na changamoto nyingi, ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa mila na desturi zenye kuleta madhara, umaskini uliokithiri, mawasiliano na miundo mbinu mibovu  ambapo husababisha hali ya maisha ya watu kuwa duni na tegemezi na hatimaye kutumia muda mwingi wa kufanya kazi bila ya kujali madhara yatakayotokea kwa familia.  Madhara haya ni pamoja na watoto kuwa na tabia mbaya kama kuacha shule, kukimbilia mitaani, kutokuwa na maadili na kuiga tamaduni zisizokubalika katika jamii yetu.
Ni wazi kuwa changamoto hizi zinaweza kushughulikiwa vyema kuanzia ngazi ya familia na ngazi mbalimbali za uongozi. Kwa kuwa maadhimisho ya mwaka huu yatafanyika kimkoa, napenda kuwaasa watanzania wenzangu kutenga muda wa kutosha kukaa na familia zao ili kujadili, kushauriana na kutekeleza masuala muhimu ya kuendeleza familia zao; kwani familia ndiyo kitovu cha maendeleo.  Aidha viongozi katika ngazi mbalimbali wahamasishe na kuhimiza watumishi wote kuona njia bora za kugawa muda wa kazi na muda wa kushughulikia familia zao ili kujenga maadili na maendeleo ya familia.  Natoa wito kwa wananchi wote kushiriki kikamilifu katika kuadhimisha siku hii kwa kuwa kila mmoja wetu ana familia na ni sehemu ya familia ndani ya  jamii.
Ni matumaini yangu kwamba kupitia maadhimisho haya familia zitakumbushwa wajibu na mchango wao katika maendeleo ya familia zao, jamii na Taifa kwa ujumla . 
Nawatakia maadhimisho mema ya Siku ya Familia Duniani.

Asanteni,


 
                                                               Anna T. Maembe
                                                               KAIMU KATIBU MKUU

No comments:

Post a Comment