Monday, May 14, 2012

Manchester City bingwa Ligi ya England




                             Wachezaji wa Manchester City wakishangilia ubingwa


Manchester City ikifunga mabao mawili zikiwa zimesalia dakika mbili za nyongeza mpira kumalizika, wamefanikiwa kuunyakua ubingwa wa Ligi Kuu ya Kandanda ya England kwa kuwalaza QPR waliocheza wakiwa 10 kwa mabao 3-2 katika mchezo uliomalioza msimu kwa mtindo wa kusisimua.
Pablo Zabaleta alikuwa wa kwanza kuipatia bao la kuongoza Manchester City kabla Joleon Lescott kufanya makosa na kumpatia nafasi Djibril Cisse kuisawazishia QPR.
Joey Barton alitolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kukwaruzana na Carlos Tevez lakini alikuwa Jamie Mackie aliyeipatia bao la pili QPR kipindi cha pili.
Huku Manchester United ikiwa imeshailaza Sunderland, Manchester City walionekana kama wangepoteza nafasi ya kuunyakua ubingwa lakini Edin Dzeko akafanikiwa kufunga bao la kusawazisha kwa kichwa na dakika moja baadae Sergio Aguero akapachika bao la ushindi lililoimaliza kabisa QPR.
Hili ni taji la kwanza la Manchester City tangu waliposhinda kombe la Ubingwa wa Ligi daraja la kwanza wakati huo mwaka 1968.
Manchester United imepoteza taji lake la Ligi Kuu ya England, licha ya kuilaza Sunderland baada ya mahasimu wao wakubwa Manchester City kuilaza Queens Park Rangers.
Bao la kichwa lililowekwa kimiani na Wayne Rooney lilioneka kama lingempatia Sir Alex Fergusonubingwa wa Ligi Kuu ya Kandanda kwa mara ya 13 kwa kipindi chake cha umeneja kwa miaka 20.
Manchester United walikuwa wanadhani wameshinda ubingwa baada ya Manchester City kuwa nyuma kwa mabao 2-1 na zikiwa zinaelekea dakika za nyongeza kumalizika huku mashabiki wao wakianza sherehe za ubingwa.
Lakini taarifa zilizofika kwa mashabiki wa Manchester United kwamba Manchester City wamepachika mabao mawili ya haraka haraka dakika za mwisho ziliwanyamazisha mashabiki hao na wachezaji wao wakaonekana hawaamini wanachokisikia.
Arsenal imefanikiwa kupata nafasi ya tatu na watacheza Ligi ya Ubingwa wa Ulaya msimu ujao moja kwa moja baada ya kuilaza West Brom mabao 3-2, hasa kutokana na makosa ya mlinda mlango wa West Brom Marton Fulop.
Ushindi huo wa 3-2 ina maana kikosi cha Arsene Wenger kimemaliza msimu wakishika nafasi ya tatu.
Fulop alifanya makosa yaliyoipatia Arsenal bao la kuongoza dakika nne tu tangu mchezo ulipoanza kupitia kwa Yossi Benayoun lakini muda mfupi tu West Brom wakafanikiwa kusawazisha.
Lakini walikuwa Andre Santos na Laurent Koscielny waliopiatia Arsenal mabao ya ushindi kwa Arsenal.
Tottenham baada ya kuilaza Fulham mabao 2-0 imefanikiwa kumaliza ligi wakiwa nafasi ya nne lakini watajipatia nafasi ya kucheza Ligi ya Ubingwa wa Ulaya iwapo tu Chelsea itapoteza mchezo wa fainali ya Ubingwa wa Ulaya.

Emmanuel Adebayor alikuwa wa kwanza kuipatia Tottenham bao la kwanza ambapo Fulham nao walikosa nafasi nzuri ya kufunga kwa mkwaju wa Moussa Dembele kugonga mwamba.
Jermain Defoe aliithibitishia Tottenham ushindi baada ya kupachika bao la pili kutokana na mkwaju wa awali alioufumua Aaron Lennon kuwagonga wachezaji wa Fulham.
Ndoto za kucheza Ubingwa wa Ulaya kwa Newcastle ziliyeyuka baada ya Everton kumaliza msimu kwa mtindo wa aina yake katika uwanja wa Goodison Park. Everton walifanikiwa kupata ushindi wa mabao 3-1.Steven Pienaar aliufungua mlango wa Newcastle kwa mkwaju wa yadi 20 ambao ulimgonga mlinzi wa Newcastle Mike Williamson na kujaa wavuni.
Nikica Jelavic akaiongezea Everton bao la pili sekunde chache baada ya jitahada zake za awali kupanguliwa na mlinda mlango Tim Krul kabla Johnny Heitinga kuongeza bao la tatu.
Chelsea kwa urahisi iliilaza Blackburn mabao 2-1 baada ya kumiliki mpira kwa muda mrefu katika uwanja wa Stamford Bridge.
Chelsea walipumzisha wachezaji wao wengi nyota wakiwa wanajiandaa kwa fainali ya Ubingwa wa Ulaya wiki ijayo, lakini hata hivyo hawakuonesha kandanda ya kuvutia sana.
John Terry aliufungua mlango wa Blackburn kwa bao la kichwa baada ya kuunganisha mkwaju wa juu uliochongwa na Romelu Lukaku na baada ya dakika tatu Raul Meireles akaifungia Chelsea bao la pili.
Chelsea walikosa nafasi nyingi za kufunga lakini Yakubu alionekana mwiba kwa ngome yao baada ya kuipatia Blackburn bao moja katika shambulio la nadra walilofanya.
Danny Graham akiwa amefunga bao lake la 100 tangu aanze kucheza kandanda alifanikiwa kuipatia Swansea ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Liverpool.
Graham alifumua mkwaju akiwa karibu na lango zikiwa zimesalia dakika nne kabla mpira kumalizika na kupata ushindi wa kumbukumbu.
Swansea walimiliki mchezo kwa muda mrefu kipindi cha kwanza na Gylfi Sigurdsson mara mbili alikosa nafasi za kufunga.
Liverpool walibadilika kipindi cha pili na Andy Carroll mpira wa juu alioupiga uliokolewa na mlinda mlango Michel Vorm.
Norwich walimaliza msimu vizuri sana baada ya kupata ushindi rahisi dhidi ya Aston Villa hali iliyoongeza chagizo kwa meneja Alex McLeish.
Mshambuliaji wa Norwich Grant Holt alikuwa wa kwanza kuipatia timu yake bao la kwanza kwa mkwaju wa adhabu ya moja kwa moja na kuandika bao lake la 17 msimu huu.

Simeon Jackson alitumia makosa ya mlinzi wa Aston Villa Carlos Cuellar na kupachika bao la pili akiwa karibu kabisa na lango.
Villa iliwalazimu wamshukuru sana mlinda mlango wao Shay Given, ambaye alifanya kazi ya ziada kupunguza mabao.
Meneja wa Aston Villa McLeish alikuwa akizomewa na mashabiki wa timu yake muda wote wa mchezo ambapo tangu ameichukua timu hiyo msimu huu mambo hayakumuendea vizuri.
Bolton hatimaye wameshuka daraja na msimu ujao hawatacheza tena Ligi Kuu ya Kandanda ya England baada ya kutoka sare na Stoke katika uwanja wa Britannia.
Iwapo Bolton wangeshinda mechi hiyo - huku QPR wakiwa wamefungwa na Manchester City -wangepona na shoka la kushuka daraja, lakini bao la mkwaju wa penalti uliofungwa na Walters likaizamisha.
Mark Davies alikuwa wa kwanza kuipatia bao Bolton na baadae bao lililofungwa na Kevin Davies likaonekana kabisa kufufa uhai kwa Bolton.
Lakini bao la penalti la Walters bada ya Peter Crouch, kufanyiwa rafu ndani ya boksi likaididimiza Bolton na msimu ujao watacheza ligi ya Championship.
Wigan imefanikiwa kupata ushindi wa saba katika mechi tisa ilizocheza na kuepuka kabisa panga la kuwateremsha daraja dhidi ya Wolverhampton Wanderers ambao tayari wameshateremka daraja. Wingan wameshinda mabao 3-2.
Bbc.

No comments:

Post a Comment