Mkuu wa mkoa wa Singida,Dk.Parseko Kone akizungumza kwenye mkutano wa wadau wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Katala Beach hoteli mjini Singida.
Mjumbe wa bodi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Lyidia Choma (kulia) akitoa taarifa yake kwenye siku ya wadau wa Mfuko huo na ule wa Afya ya Jamii (CHF).Mkutano huo ulifanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Katala Beach Hotel mjini Singida. Kushoto (aliyeshika mike) ni Meneja wa NHIF mkoa wa Singida, Agnes Chaki.
Mkurugenzi wa takwimu na uhai wa mfuko wa NHIF makao makuu, Michael Mhando akitoa nasaha zake kwenye mkutano wa wadau wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF), uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Katala Beach Hotel mjini Singida. Kushoto ni mkuu wa mkoa wa Singida,Dk.Parseko Kone, Wa kwanza kulia ni kaimu Mganga Mkuu wa mkoa wa Singida,Dk.Mussa Kamala, Mkuu wa wilaya ya Singida,Queen Mlozi na katibu tawala mkoa wa Singida,Liana Hassan.
Mkuu wa mkoa wa Singida,Dk.Parseko Kone, (wa pili kulia) akifuatilia kwa makini mada zilizokuwa zikitolewa kwenye mkutano wa siku ya wadau wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na Mfuko wa Afya ya Jamii. Wa kwanza kulia ni Mjumbe wa Bodi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Bi. Lyidia Choma.Wa tatu kulia ni Katibu Tawala mkoa wa Singida, Liana Hassan na,Mkuu wa Wilaya ya Singida,Queen Mlozi na kaimu Mganga Mkuu mkoa wa Singida,Dk.Mussa Kimala.
Na Nathaniel Limu
Zaidi ya asilimia 73 ya kaya za mkoa wa Singida, hazijajiunga na mfuko wa afya ya jamii (CHF), hali inayochangia wanafamilia watibiwe bila utaratibu maalum.
Hayo yamesemwa na mkuu wa moa wa Singida, Dk. Parseko Kone, wakati akizungumza kwenye uzinduzi wa mkutano wa siku ya wadau wa Mfuko wa Taifa Bima ya Afya na Mfuko wa Afya ya Jamii (NHIF) wa mkoa wa SIngida.
Akifafanua, amesema kati ya kaya 259,251 za mkoa wa Singida, ni kaya 45,575 tu, ndizo zilizojiunga na mfuko wa afya ya jamii kati ya mwaka 1998 na Septemba 30 mwaka huu. Hii ni sawa na asilimia 17.6 tu.
“Hata hivyo,wilaya ya Iramba imekuwa ikifanya vizuri katika uandikishaji wa wananchi, kwani takwimu zinaonyesha hadi Septemba 30 mwaka huu, wamekwisha andikisha asilimia 50.3 ya kaya zilizolengwa. Hali hii inaonyesha kuwa viongozi bado hatujatimiza wajibu wetu wa kuhamasisha wananchi kujiunga na mfuko huu”, amesema Dk.Kone.
Aidha, mkuu huyo wa mkoa, amesema pia inawezekana watoa huduma wamekuwa ni chanzo cha kuwakatisha tama wananchi waliojiunga na hivyo, kuwafanya wananchi wengine wasite kujiunga na Mfuko huu.
“Kwa kuwa wadau wote tumekutana hapa leo, ni nafasi yetu kuangalia nini sababu ya kuzorota kwa utaratibu huu ambao katika baadhi ya halmashauri hapa nchini, umeimarika zaidi",amesema Dk.Kone.
Awali mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Lyidia Choma, alisema Mfuko huo umeidhinisha shilingi bilioni 10, ili zitolewe kwa watoa huduma kuwawezesha kupata vifaa tiba na kukarabati maeneo yao ya kutolea huduma.
“Utaratibu huu ni mikopo ya bei nafuu ambayo hairejeshwi kwa fedha taslimu, isipokuwa kwa kukatwa katika madai ambayo mtoa huduma anawasilisha kwa Mfuko”,amefafanua.
Alifafanua kuwa kwa mkopo wa vifaa tiba, mkopo hurudishwa kwa makato ya asilimia 10 ambayo hulipwa ndani ya miezi 24 na mikopo ya ukarabati wa maeneo ya kutolea huduma, ni miezi 36.
Kauli mbiu ya mwaka huu, ni Afya Bora kwa wote sasa kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.
No comments:
Post a Comment