Monday, November 11, 2013
WAKIMBIZI WA SOMALIA KURUDISHWA NYUMBANI
Zaidi ya wakimbizi 500,000 wasomali wanaoishi nchini Kenya, wanatarajiwa kurejeshwa makwao Somalia, baada ya shirika la kuwahudumia wakimbizi hao la UN kutia saini mkataba na Kenya pamoja na Somalia kuhusu kuwarejesha nyumbani wakimbizi hao.
Wasomali hao watarejeshwa kwa hiari nchini Mwao katika kipindi cha miaka mitatu inayokuja.
Wasomali wamekuwa wakitafuta hifadhi nchini Kenya kutokana na vita na umasikini nchini Somalia.Kambi mbili ambako wakimbizi hao wanaishi, Dadaab na Kakuma zinafanana na miji mikubwa kwa ajili ya idadi kubwa ya wakimbizi hao.
Baadhi ya wakimbizi pia wanaishi katika mtaa wa Eastleigh mjini Nairobi ambao unajulikana kama Somalia ndogo kutokana na idadi kubwa ya wasomali wanaoishi mtaani humo.
Wakimbizi wengi kutoka Somalia walitoroka kutokana na vita, baada ya serikali kuporomoka mwaka 1991.
Wengi wao walizaliwa kambini na hawajawai kamwe kwenda Somalia.
Serikali za Kenya na Somalia pamoja na UN zimeanzisha rasmi mpango wa kuanza maisha mapya nchini Somalia na kushiriki katika mpango wa kujenga upya nchi yao.
Naibu waziri mkuu wa Somalia Fowsia Yusuf Adam, alisema Serikali inajiandaa kuwapokea raia wake waliokuwa wanaishi ukimbizini.
Umoja wa Mataifa umesema kuwa makubaliano ya kuwarejesha wakimbizi Somalia ni wito kwa jamii ya kimataifa kujitolea kutafuta suluhu la kudumu kwa mzozo ambao umeendelea kwa miaka mingi bila kikomo.
Hata hivyo changamoto ni kuwa mkataba huo unawataka wakimbizi kurejea kwa hiari ingawa wengi wanaona Somalia bado ni mahala pasipo salama na hivyo itakuwa vigumu kwao kurejea.
Toa Maoni Yako
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment