Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa
Jakaya Mrisho Kikwete ameshtushwa na kufadhaishwa na taarifa za kifo cha Mjumbe
waTume ya Mabadiliko ya Katiba, Dkt. Sengondo Mvungi kilichotokea jana,
Jumanne, Novemba 12, 2013 kwenye Hospitali ya Milpark, Johannesburg,
AfrikaKusini.
Katika salamu za rambirambi ambazo amemtumia Mwenyekitiwa
Tume hiyo, Jaji Joseph SindeWarioba, Rais Kikwete amesema kuwa amepokea kwa
mshtuko mkubwa na fadhaha taarifa za kifo cha Dkt. Mvungi. “Kwa hakika ni
taarifa iliyonisumbua na kunipa huzuni nyingi.”
Rais Kikwete amesema kuwa hakuna shaka kuwa katika maisha
yakeDkt. Mvungi ametoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Tanzania kwa namna
mbalimbali na kuwa kifo kimemfika wakati Taifa la Tanzania lilikuwa bado
linahitaji busara, hekima na mchango wake katika mchakato mzima wa kusaka
Katiba mpya.
“Kuanzia alipokuwa mwandishi wa habari katika Magazeti ya
Chama cha Mapinduzi (CCM) ya Uhuru na Mzalendo, hadi uhadhiri wake katika Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam, hadi uwakili katika Kampuni ya South Law Chambers,
hadi uongozi wake katika Chama cha NCCR-Mageuzi, hadi uamuzi wake wa kugombea
Urais wa Tanzania mwaka 2005 na sasa akiwa Mjumbe wa Tume ya Katiba, Dkt.
Mvungi ametoa mchango wake mkubwa sana katika maendeleo ya nchi yetu. Na hili
hatutalisahau,” amesemaRaisKikwete.
“Kwa masikitiko makubwa, nakutumia wewe Jaji Joseph
Warioba, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba salamu za rambirambi za
dhati ya moyo wangu nikiombeleza kifo cha Dkt. Mvungi. Nakupa pole nyingi wewe
Mwenyekiti, wajumbe wa Tume na wafanyakazi wote wa Tume kwa kuondokewa na
mwenzenu. Naungana nanyi kuombleza msibahuo mkubwa.”
“Aidha, kupitia kwako, natuma pole nyingi kwa
wana-familia, ndugu, marafiki nan majirani wa Dkt. Mvungi kwa kuondokewa na
mhimili,msimamizi wafamilia na ndugu. Wajulishe kuwa niko nao katika msiba huu
mkubwa.Wajulishe kuwa msiba wao ni msiba wangu pia. Muhimu waelewe kuwa binafsi
naelewa machungu yao katika kipindi hiki kigumu na namwomba Mwenyezi Mungu
awape subira waweze kuvuka kipindi hiki kigumu kwa sababu yote ni mapenzi
yake.”
Amemalizia Rais Kikwete: “Napenda kuungana nao katika
kumwomba MwenyeziMungu, Mwingi wa Rehema, aiweke mahali pema roho ya Marehemu
Dkt. Sengondo Mvungi. Amina.”
Wakati huo huo Rais Kikwete ametuma salamu za rambirambi
kwa familia ya Marehemu Musa Hillal Samizi ambaye alifariki tarehe 11
Novemba,2013 hapa Dar es Salaam.
Rais amemwelezea marehemu Samizi kama kada mahiri na
mtumishi mwaminifu katika uhai wake.
Rais amesema “Marehemu Samizi atakumbukwa kwa upendo,
ushirikiano na uchapakazi wake katika kazi na katika nafasi mbalimbali ambazo
aliwahi kushika ndani ya Chama cha Mapinduzi na Serikalini”.
Marehemu Samizi aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali
zikiwemo Ubunge wa Jimbo la Kigoma Mjini,Katibu Msaidizi wa Chama cha Mapinduzi
Makao Makuu Dodoma, Afisa Utumishi NBC, Mjumbe wa NEC, Mjumbe wa Bodi MECCO,
SHIHATA, Serengeti Safari Lodge pamoja na Mkuu wa Wilaya za Handeni, Kasulu,
Tabora na Moshi kabla ya kustaafu Mwaka 2012 alipostaafu.
No comments:
Post a Comment