Wanajeshi na polisi wa Ufilipino wamepelekwa
katika miji ilioathirika na kimbunga kikali kuwahi kuipiga nchi hiyo ili
kudhibiti wizi wa mali unaohatarisha juhudi za kutoa misaada ya kibinaadamu kwa
waathirika. Zaidi ya watu 10,000 wanahofiwa kufariki kutokana na kimbunga hicho
kwa jina Haiyan kilichopiga kwa mawimbi mazito na upepo mkali na kusababisha
athari kubwa nchini Ufilipino siku ya Ijumaa, huku mji wa Tacloban ukiwa moja
ya miji ilioathirika pakubwa.
Waokoaji kwa sasa wanajaribu kupeleka misaada
ya chakula na malazi kwa waathirika wa kimbunga hicho katika mji huo ulio na
idadi ya watu 220,000.
Hata hivyo hatua hiyo iliendeshwa kwa changamoto kubwa kutokana na wizi
uliokuwa ukiendelea. Waporaji walivunja maduka pamoja na kuvamia gari la
misaada la msalaba mwekundu na kuchukua vile vilivyokuwemo ndani.Baadhi ya
waathiriwa ambao ni wafanyabiashara wadogo pia wameripoti kuibiwa kwa
televisheni, na mashini za kufulia nguo. Kulingana na msemaji wa wizara ya ulinzi
wa raia nchini humo, Reynaldo Balido, kurejesha usalama na hai ya utulivu
katika mji huo wa Tacloban, ni moja ya mambo wanayoyapa kipaumbele.
Akizungumza na shirika la habari la AFP hapo
jana, Andrew Pomeda, aliye na umri wa miaka 36, na mwalimu wa shule moja ya
upili mjini humo, amesema watu kwa sasa wamegeuka kuwa wahalifu, kwa kuingia
katika majengo ya kibiashara kuiba chakula na mali. Pomeda amesema ana hofu
kwamba kwa muda wa wiki moja watu watakuwa wanauana kutokana na njaa.
Wakati huo
huo, jeshi la Marekani limeungana na wenzao wa Ufilipino kuendeleza juhudi ya
kuwatafuta manusura wa Kimbunga Haiyan. Siku nne baada ya kimbunga hicho
kuikumba nchi hiyo na kusababisha maelfu ya miili kutapakaa kote barabarani,
sasa waathirika wana mahitaji makubwa ya chakula, maji, matibabu na malazi.Joan
Lumbre-Wilson mkaazi wa mji wa Tacloban amesema kinachohitajika kwa sasa ni
kundi lililojipanga ambalo litajishughulisha na zoezi la kuondoa miili
iliyotapakaa barabarani na pia kusimamisha wizi mkubwa wa mali ya watu
unaoendelea.
Eneo jengine lililoathirika ni mji wa Samar
ambapo Gavana wa mji huo amethibitisha kuuwawa kwa watu 433 na kusema idadi
hiyo huenda ikaongezeka.
Huku hayo yakiarifiwa, watu 10 wanasemekana
kufariki, 67 wamejeruhiwa huku wengine 39,000 wakihamishiwa katika maeneo
salama baada ya kimbunga hicho Haiyan kusababisha mvua kubwa nchini Vietnam,
hasa katika maeneo ya kaskazini mashariki na katikati mwa nchi hiyo.
Toa Maoni Yako
comments
No comments:
Post a Comment