Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko Maria Bilia akizungumza na waandishi wa habari kuhusu siku ya Viwanda Afrika ambapo alielezea mafanikio na changamoto katika sekta ya viwanda nchini na Afrika kwa ujumla. Kulia ni Afisa mipango wa Taifa kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO) Bw. Gerald Runyoro.
Afisa Mipango wa Taifa kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO) Bw. Gerald Runyoro akizungumzia ushiriki wa shirika hilo katika kukuza viwanda nchini.
Kaimu Mwenyekiti wa Shirikisho la Viwanda Nchini (CTI) Dr. Samwel Nyantahe akizungumzia umuhimu wa kuongeza thamani za bidhaa zinazozalishwa hapa nchini kwa minajiri ya kupambana na tatizo la ajira.
Mkurugenzi wa Viwanda vidogo vidogo kutoka Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko Dakta. Consolatha Ishebadi (katikati) akifafanua changamoto wanazokutana nazo wafanyabiashara wazawa katika kutengeneza vifungashio vyenye ubora (Packaging) kwenye bidhaa zao.
Mwandishi kutoka gazeti la The Citizen akiuliza swali wakati wa mkutano huo wa siku ya Viwanda Afrika.
Sehemu ya waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali waliohudhuria mkutano huo.
Na Damas Makangale, Moblog
SERIKALI imesema haitasita kuwachukulia hatua kali za kisheria wafanyabiashara wote kutoka nje wanaofanya biashara au kufungua viwanda vidogo vidogo bila kufuata taratibu, kanuni na sheria za nchi. Moblog inaripoti.
Akizungumza na Waandishi wa Habari katika kuadhimisha Siku ya Viwanda Afrika jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko, Bi. Maria Bilia amesema kuna baadhi ya wafanyabiashara toka nje ambao hawataki kufuata taratibu za uwekezaji na sheria za nchi.
“Matokeo ya kutokufuata sheria za nchi katika uwekezaji au ufanyaji wa biashara ni uanzishwaji wa viwanda vinavyozalisha bidhaa ambazo hazikidhi viwango na ni hatari kwa Afya za walaji,”
“Sheria za nchi zipo wazi kwamba lazima Kituo cha Uwekezaji (TIC) na Brela msajili wa biashara wahusishwe kwenye mchakato mzima wa uwekezaji au biashara yeyote ndani ya nchi,” Bilia amesema
Amesema vile vile Wizara ya Viwanda kwa kushirikiana na Wizara zingine na taasisi za Serikali wanaendelea kurahisisha urasimishaji wa biashara kwa wanyonge kupitia mradi wa Mkurabita Mkakati wa Kurasimisha Biashara kwa Wanyonge ili kuwawezesha wazawa kufanya biashara zenye tija kwao na taifa kwa ujumla.
Bi. Bilia aliendelea kusema kuwa siku ya viwanda Afrika ilianzishwa mwaka 1989 na Tanzania ilijiunga rasmi mwaka 1990 katika kuhamasisha ukuaji wa viwanda katika kukuza uchumi wa nchi za Afrika.
Amesema sekta ya viwanda ikishirikishwa na sekta zingine inaweza kufanya mabadiliko haraka katika maisha ya mtu mmoja mmoja hususani ajira na hutoa bidhaa bora kwa matumizi ya binadamu.
Alisisitiza kuwa mwaka huu Serikali imepanga kuwa na maonyesho ya wiki nzima yatakayofikia kilele tarehe 20 mwezi huu ambapo wafanyabiashara mbalimbali watapata fursa ya kuonyesha bidhaa zao katika ukumbi wa PTA saba saba.
Amesema kauli mbiu ya mwaka huu ni “ Ni Ajira na ujasiriamali, Fursa ya Kuharakisha Maendeleo ya Viwanda Afrika katika juhudi za kupunguza makali ya umaskini na tatizo la ajira kwa vijana.
Kwa upande wake, Kaimu Mwenyekiti wa Shirikisho la Viwanda Nchini (CTI) Dkt. Samwel Nyantahe amesema shirikisho la viwanda linaunga mkono juhudi za serikali katika kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa hapa nchini ili kuongeza mapato ya nchi.
“Sisi Shirikisho la Viwanda kwa kushirikiana na serikali na watu binafsi tutaendelea kuhamasisha jamii umuhimu wa viwanda katika kuongeza thamani ya bidhaa na kupambana na tatizo la ajira nchini,” amesema
Bw. Gerald Runyoro kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO) amesema umoja wa mataifa kwa kushirikiana na serikali na wadau wengine wataendelea kusisitiza watu kuwekeza na kufungua viwanda ili kuharakisha maendeleo ya kiuchumi Afrika.
Amesema wafanyabiashara lazima wawe na ujasiri wa kufungua biashara au kiwanda katika juhudi za kuongeza thamani bidhaa zitokazo Afrika na kutafuta fursa za uwekezaji nje ya Afrika.
No comments:
Post a Comment