Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.Mohammed Gharib Bilal, akizungumza na baadhi ya Viongozi wa Selcom Wireless Tanzania, Meneja Miradi wa Selcom, Gallus Runyeta (katikati) akitoa maelezo kuhusu shughuli zinazofanywa na Selcom. (kushoto) ni Meneja Masoko na Muendesha Biashara, Juma Mgori.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.Mohammed Gharib Bilal, akizungumza na baadhi ya Viongozi wa Selcom Wireless Tanzania, Meneja Miradi wa Selcom, Gallus Runyeta (katikati) akitoa maelezo kuhusu shughuli zinazofanywa na Selcom. (wa pili kushoto) ni Meneja Masoko na Muendesha Biashara, Juma Mgori na Mhandisi wa Software, Godfrey Kiapinga.
********************************
Mheshimiwa Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal amekutana na
Uongozi wa Kampuni ya Selcomwireless Tanzania na kufanya nao mazungumzo ofisini
kwake Ikulu jijini Dar es Salaam Jumatatu Novemba 04, 2013. Uongozi wa Selcomwireless
uliofika kukutana na Mheshimiwa Makamu ulikuwa pamoja na Meneja Miradi wa
Selcom (Gallus Runyeta), Meneja Masoko na Muendesha Biashara (Juma Mgori) na Mhandisi
wa Software (Godfrey Kapinga).
Wakiwa katika
mazungumzo na Mheshimiwa Makamu wa Rais, Meneja Miradi wa Selcomwireless Tanzania
Gallus Runyetta alimueleza Mheshimiwa Makamu wa Rais kuwa, kampuni yao ambayo
imejikita katika kutoa huduma za malipo ya Kielekroniki imekuwa ikifanya miradi
mbalimbali ambayo imerahisisha malipo kwa wananchi wa Tanzania ikiwa ni pamoja
na malipo ya umeme wa Luku na sasa iko katika hatua za mwisho za kuzindua ushirikiano
na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhusu uthaminishaji wa malipo ya magari
hali ambayo itasaidia kupunguza usumbufu kwa wanaoagiza magari nje ya nchi.
Uongozi wa Selcomwireless
pia ulimueleza Mheshimiwa Makamu wa Rais kuwa, Selcom inazidi kujitanua katika
kutoa huduma za malipo sambamba na takwimu katika maeneo ya afya na mfano mzuri
ni Zanzibar ambako huko Selcomwireless imeshiriki katika harakati za kutokomeza
Malaria, harakati ambazo pia inashiriki kwa upande wa Tanzania Bara.
Mheshimiwa Makamu wa
Rais aliwataka Selcomwireless kuendelea kuisaidia nchi hasa katika suala zima
la kukusanya mapato na akawataka kuhakikisha wanakutana na Uongozi wa Mfuko wa
Bima ya Afya ili kuwapa namna ya kusaidia wananchi hasa wa vijijini kulipia
Bima zao kwa gharama wanazoweza kumudu.
“Mkiwasaidia watu wa
Bima ya Afya na kuwafanya walipaji kuwa wanalipa kidogo kidogo kwa vipindi
fulani inaweza kabisa kubadili hali ya huduma za afya hapa nchini,” alisema na
kuongeza: “Tunakutegemeeni sana na jitahidini kutumia nafasi hizi ili
kuhakikisha kuwa wananchi wengi wanajitokeza kulipia Bima za afya kwa
kuwarahisishia namna ya kupata huduma”.
Mheshimiwa Makamu wa
Rais pia aliwataka Selcomwireless kutafuta namna ya kutatua changamoto ya
ulipaji wa kodi za nyumba sambamba na kukutana na viongozi wa Wizara ya Ardhi,
ili watu walio na Hati zao za viwanja na makazi waweze kulipa kodi zao kwa
mtandao ili kurahisisha ukusanyaji na pia kutanua wigo wa mapato katika manispaa
hapa nchini.
Imetolewa na: Ofisi ya Makamu wa Rais
Ikulu, Dar es Salaam
Jumanne 05, 2013
No comments:
Post a Comment