Rais Jakaya Kikwete (katikati) akibadilishana mawazo na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba (kushoto) nyumbani kwa marehemu Dkt. Sengondo Mvungi walipokwenda kuipa pole familia. Kulia ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi James Mbatia na Mjumbe wa Tume Waziri Mkuu Mstaafu Dkt. Salim Ahmed Salim.
Tume ya Mabadiliko ya Katiba inawafahamisha wananchi kuwa
taratibu za kuusafirisha mwili wa Mjumbe wake, Dkt. Sengondo Mvungi aliyefariki
nchini Afrika Kusini zimekamilika na mwili wake unatarajia kuwasili nchini siku
ya Ijumaa, Novemba 15, 2013.Baada ya kuwasili, mwili huo utahifadhiwa katika
Hospitali ya Jeshi Lugalo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Aidha, siku ya Jumamosi, Novemba 16, 2013 kutafanyika
Ibada ya mazishi katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph jijini Dar es
Salaam kuanzia saa 4:00 asubuhi. Baada ya misa, marehemu ataagwa katika Viwanja
vya Karimjee kuanzia saa 6:30 mchana siku hiyohiyo ya Jumamosi, Novemba 16,
2013.
Aidha, Marehemu Dkt. Mvungi anatarajiwa kusafirishwa siku
ya Jumapili, Novemba 17, 2013 kwenda Kisangara Juu, Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro
kwa ajili ya mazishi yanayotarajiwa kufanyika siku ya Jumatatu, Novemba 18,
2013.
Dkt. Mvungi alifariki jana (Jumanne, Novemba 12, 2013)
katika Hospitali ya Millpark jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini
alikopelekwa kwa ajili ya uchunguzi na matibabu zaidi akitokea Kitengo cha
Mifupa Muhimbili (MOI) aliokuwa amelazwa baada ya kuvamiwa nyumbani kwake
Kibamba, wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam na watu waliomjeruhi vibaya
kichwani usiku wa kuamkia siku ya Jumapili, Novemba 3, 2013.
Wakati huohuo, Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba
wakiongozwa na Mwenyekiti wake Jaji Joseph Warioba leo (Jumatano, Novemba 13,
2013) wameungana na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.
Jakaya Mrisho Kikwete kufika nyumbani kwa marehemu Dkt. Mvungi eneo la Kibamba
jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kutoa pole kwa familia, ndugu na jamaa wa
marehemu Dkt. Mvungi.
No comments:
Post a Comment